21 July 2011

Spika ambana Waziri Mkulo

*Wataka majina waliochukua mabilioni kufufua uchumi

Na Gladness Mboma, Dodoma

SPIKA wa Bunge, Bi. Anne Makinda amemtaka Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo kuyataja bungeni kampuni 97 zilizonufaika na mpango wa
kunusuru uchumi wa Tanzania kutokana na msukosuko wa fedha duniani.

Spika Makinda amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Bw. Pereila Ame Silima kushindwa kujibu maswali ya Mbunge wa Hai, Bw. Freeman Mbowe na mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Leticia Nyerere waliotaka kutajiwa kampuni hizo.

Katika swali la msingi, Bi. Nyerere alitaka kujua ni kampuni ngapi, kwa majina na kiasi gani cha fedha zilizotumika kwa ajili ya kunusuru uchumi wa Tanzania katika kipindi cha mtikisiko wa uchumi wa dunia na fedha hizo zilitoka wapi na kiasi gani kwa kila chanzo.

Pia mbunge huyo alitaka kujua kama kampuni hizo zilipewa mkopo au msaada; na kama ni mkopo ni lini zitaaza kulipwa.

Pia alihoji fedha kiasi gani zimetumika hadi kufikia Desemba mwaka jana na kwa kuwa ni fedha za umma zinazokaguliwa na CAG, ukaguzi wake utafanyikaje kwa kuzingatiwa kuwa fedha hizo zilitolewa kwa kampuni binafsi.

Akijibu maswali hayo, Bw. Silima alisema hawezi kuyataja makampuni hayo kwa kuwa ni kuvunja utaratibu kwa kuwa ni siri kati ya benki na mteja.

Katika swali lake la nyongeza, Bw. Mbowe alihoji ni kwa nini kampuni hizo zisitajwe ikiwa zimenufaika na mamilioni ya fedha katika mpango huo, na baadaye Spika Makinda akamtaka Bw. Mkulo kutaja kampuni hizo bungeni, lakini hakueleza ni lini atatakiwa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2009/10, fedha dola milioni 48, ambazo ni sehemu ya sh. trilioni 1.7 zilizopitishwa na bunge mwaka 2008, kwa ajili ya mpango wa kufufua uchumi, hazijulikani ziko wapi, ambapo alisema wazi kuwa aliomba taarifa juu ya fedha hizo akanyimwa.

Baada ya kutoa taarifa hiyo na kuiwasilisha katika mkutano wa bunge la Aprili, suala hilo liliibuliwa bungeni, ambapo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Kabwe Zitto, alimuuliza swali la nyongeza Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda juu ya mahali zilipo fedha hizo, na kujibiwa kuwa kuwa wakati huo hakuwa na taarifa, huku Spika Anne Makinda naye akimtetea kuwa hastahili kulijibu.

Awali, akijibu swali la msingi la Nyerere, Bw. Silima alisema kupitia mpango huo kampuni 97 zilinufaika kwa kusaidiwa kufidia hasara waliyopata wakati wa msukosuko wa uchumi.

Alisema mpango huo ulikisiwa kugharimu sh. trilioni 1.7 kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi.

Alivitaja vyanzo hivyo kuwa ni mikopo ya ndani sh bilioni 828 ili kufidia pengo la mapato na sh. bilioni 436.2 zikiwa ni mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na sh. bilioni 428.3 zilitengwa ndani ya bajeti ya serikali kwa ajili ya kulinda ajira, kipato, kuwezesha utoaji mkopo na uwekezaji katika miundombinu na kuongeza kuwa urejeshwaji wa mikopo hiyo utafanywa kwa mujibu wa mikataba iliyoingiwa.

“Kutokana na kanuni za kibenki, si sahihi kutoa taarifa za mteja mmoja mmoja kwa umma kama ambavyo swali la mbunge lilivyotaka,” alisema.

Alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana fedha zilizokuwa zimetumika chini ya mpango huo zilifika sh. trilioni 1.4535 pengo likiwa ni sh bilioni 239.

“Pengo hili lilitokana na kukosekana kwa fedha kutoka katika baadhi ya vyanzo pamoja na wafadhili mbalimbali. Kwa kuwa fedha hizi ziliingizwa kwenye bajeti ya serikali zitafanyiwa ukaguzi na CAG kama ilivyo kwa fedha nyingine za umma,” alisema.

aliomba mwongozi, kwa nini hawataki kutaja...spika alimtaka hizo kampuni bunge.

3 comments:

  1. Hizo hela za Stimulus package ni CCM wameiba ili kuhonga wapiga kura katika uchaguzi mkuu 2010. Msisimbue vichwa 2005 waliiba kupitia Kagoda this time ni kwenye stumulus package ushaidi ninao

    ReplyDelete
  2. MADAKO HUNA LOLOTE USHAHIDI UNAO UTOE, UNACHOFICHS NI NINI? UNAFIKI KAMA JIMAMA VILE. WEKA NA TOA MAONI YANAYOELEKA SIYO PUMBA NA UZANDIKI UNAOTAKAM KUTUELEZA HAPO JUU.

    ReplyDelete
  3. NAFIKIRI HAPA MAKINDA AENDELEE KUMBANA MKULO ATOE ORODHA YA MAKAMPUNI YALIYOPEWA FEDHA HIZI SIO SIRI .
    MAMBO YA KIBENKI YATABAKI KUWA YA KIBENKI LAKINI KUNA MASWALA YA WAZI AMBAYO WAPIGA KURA WANATAKIWA WAYAFAHAMU NA NDILO SWALA LA MSINGI LA SWALI LA MH MBUNGE NA CC WANANCHI TUJUE PIA.

    ReplyDelete