Na Addolph Bruno
WADAU wa mchezo wa ngumi nchini wameombwa kuhudhuria mkutano wa wazi wa kimataifa unaohusu mchezo huo utakaofanyika Agosti 18 hadi 21, jijini Lusaka , Zambia.Mkutano
huo umedhaminiwa na Muungano wa Vyama vya Ngumi Afrika, unaofahamika kama African Boxing Union (ABU) na kuandaliwa na wenyeji wa mkutano, Chama cha Ngumi Zambia (BBZ).
Akizungumza na Majira kwa simu juzi akiwa mjini Iringa, Makamu wa Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), ambao ndio waratibu wa mkutano huo nchini, Fistus Luisa, alisema kutakuwa na semina kwa wasiokuwa na mafunzo ya kutosha ya mchezo huo.
"Hii ni nafasi kubwa sana kwa wadau wa ngumi barani Afrika kujifunza kupunguza matatizo tuliyokuwa nayo katika ngumi, tunaomba wadau wakiwemo makocha, waamuzi, mabondia wa sasa na wa zamani na vyama tukashiriki," alisema.
Alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka BBZ, gharama za kwenda na kurudi hoteli na matumizi mengine, zinafikia dola 600, sawa na 840,000 za kitanzania.
Makamu huyo alisema mkutano utahudhuriwa na Rais wa ABU ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Chama cha Ngumi cha Dunia (WBC), Hausin Hauchi, Katibu Mkuu wa ABU, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Ngumi cha Uganda (UPBC), Selestino Mindra.
Alisema TPBO inaratibu maombi ya wadau watakaohudhuria au katika anwani ya BBZ ambao ni waandaaji, mwisho wa kuthibitisha kushiriki umepangwa kuwa Julai 30, mwaka huu.
Akizungumzia mkutano huo, Rais wa TPBO, Yassin Abdallah 'Ustaadhi', alisema ni muhimu kwa nchi kama Tanzania kushiriki mkutano huo.
"Tunatambua kuwa watanzania wengi hali ya kifedha sio nzuri, lakini tunawahakikishia mkutano huu ni muhimu sana, na watakaohudhuria watapata somo zuri sana," alisema Yassin.
No comments:
Post a Comment