17 June 2011

Tutaandamana hata usiku na mchana-CHADEMA

Na Tumaini Makene

MAANDAMABO ya mara kwa mata yanayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwasilisha hisia juu ya masuala mbalimbali
yanayoendelea nchini yameendelea kuibua mjadala bungeni, huku wabunge wa chama hicho wakitetea msimamo huo wakisema wataandamana usiku na mchana mpaka kieleweke kwa serikali kukubali kuwajibika kwa wananchi walioichagua.

Katika michango yao, juzi na jana, katika mjadala wa bajeti unaoendelea tangu Jumatano, baadhi ya wabunge wa chama hicho walitoa kauli hizo ambazo zilionekana kuwajibu wachangiaji wenzao kutoka vyama vingine, hasa CCM ambao wamekuwa wakiwabeza kila mara wanaposimama kuchangua bajeti.

Akitoa mchango wake juzi, Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee alisema kuwa serikali ya CCM imeshindwa kutimiza wajibu wake kwa umma, hasa kwa kushindwa kuondoa umaskini na pengo kubwa la kipato linalozidi kuongezeka kati ya walionacho na wasionacho, akionya kuwa hali hiyo ikiendelea ni hatari na haitawafanya watu washindwe kuandamana kudai haki na usawa katika nchi yao.

Aliongeza pia kuwa serikali hiyo pia imeshindwa kutimiza wajibu wake kwa kutotimiza ahadi ambazo imekuwa ikitoa kwa wananchi kama vile kutengeneza ajira, hivyo isione ajabu wananchi wanapoanza kuichoka, kwa kupaza sauti na hisia zao kwa kukubali kuandamana kuipinga hadharani.

"Mlisema mtaongeza ajira...mtapunguza umaskini, lakini takwimu zinaonesha kuwa pengo la walionacho na wasionacho linazidi kuongezeka kuwa kubwa, mpaka Oktoba mwaka 2010 maskini walikuwa milioni 11 lakini mpaka sasa mwaka 2011 maskini wameongezeka kwa milioni tatu...mpaka sasa vijana vijana ni asilimia sitini lakini asilimia 14.6 hawana ajira.

"Leo wanafunzi wa UDOM wameandamana mliwaahidi mtawapatia fedha za field (mafunzo kwa vitendo), lakini hamjawapatia...tekelezeni wajibu wenu...sasa nasikia hata kule education (elimu) hawana fedha wanatakiwa kwenda mafunzo na fedha hawana, sasa kwa nini wasiingie mtaani, wakiingia mtaani mnasema CHADEMA wamewambia...tekelezeni wajibu wenu, tutaandamana mpaka kieleweke, mpaka mtakapotekeleza wajibu wenu," alisema Bi. Mdee.

Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema akichangia bajeti hiyo, pamoja na masuala mengine ya kitaifa juu ya hali ya uchumi na umaskini nchini, alisema kuwa CHADEMA wataendelea kuandamana iwe usiku ama mchana, kuhakikisha amani ya nchi inapatikana kwa wananchi kupata haki na fursa sawa ndani ya nchi yao.

Bw. John Mnyika (Ubungo) alisema kitendo cha serikali kuondoa tozo pekee katika mafuta na kushindwa kuzigusa kodi zake ambazo ndizo hasa zinaongeza bei ya mafuta nchini, alisema haitasaidia kuleta unafuu wa maisha katika bei kama serikali inavyosema, kwani hata kama bei itashuka itakuwa ni kwa kiwango kidogo takriban asilimia 1 au 2, hivyo hataunga mkono mpaka serikali itoe maelezo ya kina.

Pia walisema kuwa maendeleo yaliyofikiwa mpaka sasa hayalingani na miaka 50 ya uhuru na rasilimali ambazo nchi imebarikiwa kuwa nazo, wakisema hiyo inatokana na chama kilichokabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi kwa muda wote huo kushindwa kutimiza wajibu wake kama ilivyotarajiwa na wananchi wengi.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bi. Kidawa Salehe Hamid akichangia bajeti hiyo, ambayo aliisifia kuwa ni nzuri, alisema kuwa ni hatari kwa serikali kuendelea kutegemea mapato yanayotokana na vilevi au mvinyo na uvutaji, ambavyo huongezwa kodi karibu kila mwaka wa bajeti, huku serikali ikishindwa kubuni na kuongeza vyanzo vingine vya mapato, kama vile kutoza makampuni yanayojihusisha na uwekezaji mkubwa nchini.

"Iko siku hawa watu watashindwa halafu wataamua kugeukia kunywa pombe haramu kama gongo, ambazo huko Kenya tumeona zimeanza kuwaathiri wengine wanapofuka macho. Serikali haiwezi kuendelea kutegemea bajeti yake katika pombe na sigara...tuwatoze wawekezaji wakubwa," alisema Bi. Kidawa.

Jana Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika alikataa kuunga mkono bajeti hiyo mpaka serikali itakapotoa maelezo ya kina, juu ya masuala kadhaa, akitia mkazo katika ongezeko la tozo kwa adhabu ya makosa ya barabarani, akisema kuwa inalenga kumuumiza mtanzani wa kawaida kwani litaongeza mianya ya rushwa.

Bi. Ester Bulaya wa CCM Viti Maalumu alisema kuwa serikali inapaswa kuwa makini katika utekelezaji wa vipaumbele vyake hasa katika suala la bajeti ya umeme, akisisitiza suala la serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme kwa kutegemea bajeti yake kutokana na vyanzo vya ndani, badala ya kusubiri kutoka kwa wahisani nje ya nchi.

Bw. Hamad Masauni Yusuf wa CCM alisema kuwa kwa ujumla bajeti ni nzuri na akaiunga mkono, lakini akasisitiza suala la uwasimamizi na uwajibikaji katika kuitekeleza, akisema mtu yeyeote atakayezembea awajibike au kuwajibishwa mara moja, bila kuonewa haya.

Wabunge wengi wa kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga walitoa kilio cha njaa kubwa katika maeneo yao kama vile katika Jimbo la Solwa, Kwimba na Shinyanga, wakieleza kuwa hali ni mbaya, wakihitaji msaada wa haraka kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kiasi cha mmoja wao, Mbunge wa Solwa, Bw. Ali Salim kurudia mara nne kauli kuwa "njaa..suala la njaa kwenye Jimbo la Solwa ni kubwa sana. It is an emergency."

Mbunge huyo aliongeza "wananchi sasa hawaoni ladha ya maendeleo kwa sababu ya njaa. Waziri Mkuu lichukue hili, mwananchi wa Solwa akifa basi tena, mimi nimeshaliwasilisha kwako."

No comments:

Post a Comment