20 June 2011

Tisa marufuku kulima tumbaku

Na Sammy Kisika, Mpanda

CHAMA cha Wakulima wa Tumbaku cha Ukonongo katika Tarafa ya Inyonga, wilayani Mpanda Mkoa wa Rukwa, kimewapiga marufuku  wakulima tisa wa
zao hilo baada ya kubainika kufanya udanganyifu kwenye minada, ambapo ilibainika kuchanganya tumbaku safi na chafu.

Mkurugenzi wa Bodi ya Chama cha Ushirika cha Ukonongo, Bw. Amos Kayega, aliliambia gazeti hili kuwa uamuzi wa kuwazuia wakulima  hao kutojihusisha na kilimo hicho, umetokana na kikao cha bodi hiyo, ambacho kilijadili adhabu dhidi yao baada ya kubainika walifanya udanganyika katika minada miwili tofauti.

Bw. Kayega alisema kuwa mtindo wa kuchanganya tumbaku safi na chafu kwenye marobota ya kuuzia tumbaku maarufu kama ‘Ngulai’ ulishapigwa marufu na adhabu yake ni kuzuiwa kujihusisha na kilimo cha tumbaku kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Alisema licha ya chama chake kutoa onyo hilo mara nyingi, lakini wakulima hao walishindwa kutekeleza masharti hayo ambapo katika msimu wa mwaka huu walikamatwa wakifanya udanganyifu huo katika minada iliyofanyika kwenye vijiji vya Kamsisi, Mapili, uzega, Mgombe, Mtakuja, Nsenkwa na Inyonga.

Wakulima waliopewa adhabu hiyo ya kutojihusisha na kilimo hicho kwa mwaka mmoja kuwa ni Bw. Pius George, Bw. Gudence Mlele, Bw. Japheth Stanslaus, Bw. Paul Alfredy na Bw. John Kizo.

Wengine ni Bw. Marius Paul, Bw. Sadock Matata, Bw. Noel Alphonce na Bw. Abel Revocatous.

No comments:

Post a Comment