20 June 2011

Raia wa Kenya, Italia mbaroni kuwa 'utapeli'

Na Said Njuki, Arusha

JESHI la Polisi mkoani hapa linamsaka raia wa Kenya, Bw. Jamal Abdulwadood kwa kosa la kujipatia mali zenye thamani ya mabilioni ya fedha kwa njia ya
utapeli.

Pia jeshi hilo likimshikiliwa raia mwingine wa Italia, Bw. Pattrizio Icioni kwa kuhusishwa na tuhuma hizo za kujipatia mali za mabilioni ya fedha kwa ya udanganyifu.

Sambamba na watuhumiwa hao pia raia wengine wawili wa Kenya, Bw. Ally Said Baswabra na Bw. Amin Abdulwadood, na Mtanzania mmoja, Bw. Victor Mollel, wote kwa pamoja wanashikiliwa na jeshi hilo kwa takribani mwezi moja sasa kwa tuhuma za kujipatia mali hizo kutoka kampuni ya Salex Limited ya jijini.

Pia katika sakata hilo, pia raia mwingine wa Kenya, Bw. Vitalis Obara, anayedaiwa kuwa ni mshirika katika tuhuma hizo alishakamatwa na jeshi hilo na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha hivi karibuni, Bw. Thobias Andengenye, zinaeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya Mkurugrnzi wa Kampuni ya Salex Limited, Bw. Salim Ally kutoa malalamiko juu ya kuwepo kwa upotevu wa idadi kubwa ya ngozi mali ya kampuni hiyo.

Ngozi hizo zinazodaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 10 sawa na sh bilioni 15 za Tanzania.

Kamanda Andengenye alikiri kupata malalamiko hayo na kusema; "Tulipata malalamiko hayo na kufanikiwa kuwanasa watuhumiwa hao ambao ni raia mmoja wa Italia, Pattrizio Icioni, Ally Basabra na Amin Abdulwadood wote raia wa Kenya na Mtanzania, Bw.  Victor Mollel anayesadikiwa kuwa mhasibu wa kampuni ya Salex Limited na bado tunamsaka raia mmoja wa Kenya, Jamal Abdulwadood.

No comments:

Post a Comment