Na Peter Mwenda
JESHI la Polisi nchini halitawavumilia askari wachache watakaotumia uchache wa vizuizi katika barabara ya Dar es Salaam-Rusumo kukiuka maadili ya kazi kwa
kudai rushwa.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Bw. Mohamed Mpinga alisema jana kuwa jeshi la polisi katika kukabiliana na hali hiyo wameandaa kampeni maalumu ya kuwelimisha madereva haki na wajibu wao wanaposimamishwa na askari polisi.
Bw. Mpinga alisema jeshi hilo linawaomba madereva kutambua haki zao na kutekeleza wajibu wao wawapo barabarani ili kuondoa rushwa kwa baadhi ya askari wasio waaminifu.
Alisema Jeshi la Polisi kushirikiana na Kampuni ya Investment Climate Facility for Africa (ICF) limebuni mradi wa kuharakisha na kuhakikisha usalama wa mizigo inayosafirishwa kwenye barabara kuu za nchini.
Kamanda Mpinga alisema katika mradi huo Jeshi la Polisi limepunguza vizuizi kutoka 54 hadi 14 katika barabara kuu ya Dar es Salaam hadi Rusumo ambako magari yote yataasimamishwa na kukaguliwa katika vituo maalumu vilivyoainishwa katika kila mkoa kuwa havizidi viwili.
Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Mizani ya Uwanja wa Taifa (Dar es Salaam), Katika Mkoa wa Pwani ni Mizani ya Kibaha, Mkoa wa Morogoro (Mizani ya Mikese na Kituo cha Forodha Dumila), Mkoa wa Dodoma (Pandambili na Mizani Nala),Singida (Mizani ya Nyuki na Misigiri), Tabora (Igunga na Nzega), Shinyanga (Mizani ya Mwendakulima na Ushirombo) na Kagera ni (Nyakanazi na Mizani ya Nyakahura).
Alisema kila kituo kitakuwa na askari wasiozidi watano ambao watakuwa mchanganyiko wa idara mbalimbali na gari litakalokaguliwa kituo kimoja halitatakiwa kukaguliwa hadi kituo kinachofuata labda inapolazimika kufanya hivyo kwa sababu ya dharura na dereva kujulishwa sababu hizo.
No comments:
Post a Comment