10 June 2011

DC Motema Pemba kutua kimya kimya

Na Elizabeth Mayemba

KLABU ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), imepanga kutua nchini kimya kimya ambapo hadi jana wenyeji wao Simba walikuwa hawana
taarifa.

Timu hizo zinatarajia kucheza keshokutwa mchezo wao wa Kombe la Shirikisho (CAF), mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' alisema hadi jana wapinzani wao walikuwa hawajawapa taarifa za kutua nchini.

"Sisi tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu wa keshokutwa, lakini wapinzani wetu DC Motema Pembe hawajatupa taarifa kutuarifu lini wanatua nchini," alisema Kaburu.

Alisema kikosi chao kipo kamili na kocha wao Moses Basena, amewapika vizuri wachezaji wake, hivyo wanatarajia kushinda mchezo huo.

Kaburu alisema maandalizi hayo pia ni kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa baada ya wiki moja, ambapo Alhamisi ijayo timu yao itaondoka kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa ajili ya mchezo huo.

Aliwataka mashabiki wa soka nchini wafike kwa wingi uwanjani, ili kuishangilia timu yao na kuwataka mashabiki wawe wazalendo.

Viingilio katika mchezo huo VIP A sh. 20,000, VIP B, C sh. 10,000, viti vya orange sh. 8,000 na viti vya kijani na bluu sh. 5,000 na tiketi zitaanza kuuzwa leo.

No comments:

Post a Comment