Na Rabia Bakari
WAKILI Mabere Marando anayemtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na mwenzake Grace Martin amewasilisha maombi mawili
mahakamani na kufanya wateja wake wasianze kujitetea.
Kesi hiyo ambayo ilitajwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea, badala yake Bw. Marando akadai ana kusudio la kuwasilisha maombi mawili, na hivyo kuitaka mahakama isianze kusikiliza ushahidi wa washtakiwa.
Maombi ya Bw. Marando ni pamoja na kuitaka mahakama iingize kwenye jalada la kesi hiyo utetezi wa maandishi wa shahidi wa pili ambaye ni Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Bw. Benjamin Mkapa ambao umeandaliwa kwa njia ya kiapo.
Bw. Mkapa ni shahidi wa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo.
Pia Bw. Marando alitaja ombi la pili kwa mahakama, kuwa iwapatie mwenendo wa kesi hiyo ili waweze kwenda kuandaa utetezi kwa kuwa mwenendo ambao walipewa awali una makosa ya kimaandishi.
Hakimu Mkazi Elvin Mgeta, alisema kuhusu ombi la kwanza hauikuwa muda mwafaka kwa mahakama na pande zote mbili kuanza kuzungumzia kiapo cha Bw. Mkapa kwa kuwa hata washtakiwa wenyewe bado hawajaanza kujitetea.
Aliutaka upande wa utetezi kuwasilisha ombi hilo baada ya washtakiwa kuanza kujitetea. Wakili Mabere anasaidiana na Wakili Bw. Alex Mgongolwa kuwatetea washtakiwa katika kesi hiyo.
Kuhusu ombi la pili Hakimu Mgeta alikubaliana nalo na kuahidi ifikapo Ijumaa watakuwa wameshapewa mwenendo huo.
Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Ponsian Lukosi aliiomba mahakama itoe mwongozo kwani mawakili wa kesi hiyo wameanza kusahau matakwa ya taaluma ya sheria, kwa kutoa vielelezo vya ushahidi kwenye vyombo vya habari kabla havijawasilishwa mahakamani.
Akijibu hoja hizo, Bw. Marando, alieleza kushtushwa kuona hati hiyo kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kwani yeye ndiye aliyeandaa hati hiyo ya kiapo cha Bw. Mkapa lakini kabla ya kukiwasilisha mahakamani aliwasilina na baadhi ya maofisa wa serikali.
Alidai mahakamani hapo kuwa serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa jambo hilo kwani alidai ndio waliovujisha kiapo hicho, kwa kuwa iliandaliwa kwa siri kubwa.
Hata hivyo, Hakimu Mgeta alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kuwa kwa mamlaka aliyonayo hawezi kutoa mwongozo wala onyo lolote kuhusiana na maombi hayo.
Aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 24 mwaka huu itakapotajwa na itaendelea Julai 8 na 11 mwaka huu.
Kesi hii inaweka wazi kabisa jinsi vyombo vya Dola vilivyokuwa na UOZO.Kesi hii sasa ina umri wa mtoto kuanza shule tangia ianze. Mlalahoi akiiba nyanya sokoni anahukumiwa hapo hapo kwa kupigwa mpaka afe.Polisi watakuwa pembeni wanashuhudia tukio. Mungu ibariki CCM, Chama Tawala!!
ReplyDelete