*Yaipoza TP Mazembe kiaina
Na Elizabeth Mayemba
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeivurugia Simba mipango yake ya kuwatumia wachezaji Mbwana Samatta na Patrick Ochan katika
mechi ya Klabu Bingwa Afrika, dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco Jumamosi Jijini Cairo kwamba hawana uhalali.
Hatua hiyo ya CAF, inaonekana ni kutaka kuipoza timu ya TP Mazembe ambayo ilienguliwa na shirikisho hilo kwa kumchezesha mchezaji asiyestahili, kwa kuwa wachezaji hao wanaonekana kuwa na sifa za kuichezea Simba.
Simba kupitia TFF ilitaka kufahamu kwa CAF
kama inaweza kuwatumia wachezaji hao kwa vile Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC), kuichezea TP Mazembe bado haijatolewa.
Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kwa mujibu wa CAF, wachezaji hao hawawezi kuichezea Simba kwa vile tayari wameuzwa hivyo
kutokuwa na sifa ya kuwa wachezaji wa timu hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 26(1) ya
Kanuni za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alisema sifa ya mchezaji kwa mujibu wa kanuni hiyo ni kuwa na leseni iliyotolewa na
Chama cha Mpira wa Miguu cha nchi yake na leseni ya CAF.
Sifa nyingine anayotakiwa kuwa nayo ni kwamba awe anaichezea timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa kwenye ligi ya nchi husika na awe anaishi katika nchi iliyopo timu anayoichezea.
Hata hivyo kutokana na sifa hizo, inaonekana kwamba wachezaji hao wanazo sifa zilizotajwa katika kanuni hizo za CAF.
Wawakilishi hao wa Tanzania wanatarajia kuondoka leo usiku kwenda Cairo, Misri kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa katika Uwanja wa Petrosport.
Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi wa Misri Farouk Mohamed, ambaye atapuliza filimbi akisaidiwa na Mohamed Waleed na Hassan Sherif wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Omar Fahim, huku Kamishina atakuwa Magdy Shams el Din kutoka Sudan.
No comments:
Post a Comment