07 December 2010

Mabinti 160 wakimbia kukeketwa

Na Tumaini Makene, Mara

WAKATI viongozi na taasisi mbalimbali wakianza kushtuka na kutoa kauli za kupinga vitendo vya ukeketaji vinavyoendelea mkoani Mara, watu wa maeneo hayo wanaendelea na shughuli hiyo bila wasiwasi wowote.Wakati shughuli hiyo ikiendeshwa kwa kasi
sasa, ikiwa imeanza Novemba 12, ikitarajiwa kwenda mpaka Januari 15, mabinti takribani 160 wamelazimika kukimbia makazi yao, kwenda kuishi katika kituo maalumu wanakopewa elimu ya tohara mbadala, mpaka muda wa ukeketaji umalizike.

Kwa Mara wakati huu ambao shule zimefungwa, ni msimu wa kuendesha shughuli hiyo ambayo wengi wao, kwa mujibu wa mila zao, wanaamini kuwa ni moja ya vitendo vya muhimu, kufanyiwa wasichana na wavulana waliofikia umri wa kuingizwa utu uzima, ili wakubalike na wawe sehemu ya jamii.

Jana Majira limeshuhudia sherehe za makundi mbalimbali zikifanyika hadharani kuwapongeza na kuwatuza mabinti waliotoka kukeketwa punde, huku damu zikiwachuruzika miguuni kutokana na tohara waliyofanyiwa.

Eneo la takribani kilometa 3, nje kidogo ya Mji wa Tarime, kuanzia eneo liitwalo Nkende, kuelekea Sirali, makundi ya watu, waume kwa wake, wakiwa na marungu, wengine sime, yalikuwa yakielekea kunakofanyika shughuli za tohara.

Makundi ya namna hiyo pia, yalikuwa yakitokea Sirali, kwa shangwe na nderemo kwenda katika shughuli hizo, ambazo zilikuwa zikifanyika maeneo ya vichakani, nje kidogo kati ya Tarime Mjini na Sirali. Majira lilikuwa moja ya vyombo ya habari vilivyoweza kushuhudia mabinti wadogo kati ya miaka 12-15, wakionekana kuwa na nyuso za machungu, huku damu zikiwachuruzika, wakiwa wameweka barabarani, ili wapate pongezi zao, mara baada ya kukeketwa.

"Leo tutawafanyia wengi mno, takribani mia," alisema kwa furaha bibi mmoja ambaye jina lake halikupatikana baada ya kufika katika gari walilokuwemo waandishi wa habari kuchukua fedha ya kwenda kumtuza mmoja wa mabinti waliokeketwa.

Njia nzima kutoka eneo la Nkende mpaka karibu na Sirali, mabinti wakiwekwa katika makundi ya watu takribani watano hadi wanane, walikuwa 'wametandazwa' njiani, wamezungukwa na watu wa umri tofauti, huku ngoma maarufu ya Litungu ikipingwa kuwapongeza.

Waandishi wa habari waliweza kupata fununu kuwa tohara hiyo ambayo ni kinyume cha sheria, ilikuwa ikiendeshwa kilometa chache kutoka hapo barabarani, kwenda maeneo ya wazi yaliyokuwa nyuma ya vichaka vilivyoko kandokando
ya barabara ya Tarime-Sirali.

Uwezekano wa kugundua mahali hapo na pia kuendelea na kazi kwa amani, ulishindikana baada ya baadhi ya waandishi kuanza kuhojiwa 'wewe ni mtoto wa nani' baada ya kugundulika kuwa si wakazi wa maeneo hayo na sherehe hizo haziwahusu.

Hata hatua hiyo ya kuuliza uliza, zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu vijana wa kiume, ambao mara nyingi wamekuwa wakionekana kubeba sime katika shughuli hizo,kwa ajili ya ulinzi, walikuwa hawajafika kwa wingi maeneo hayo.

Wakati shughuli hiyo ikiendelea maeneo hayo, kilometa kadhaa kutoka mjini, katika Kijiji cha Masanga, watoto wapatao 160 wamelazimika kukimbia makazi yao, ili kukwepa kukeketwa, wakihifadhiwa katika kituo cha Kanisa Katoliki.

Wakati shughuli hiyo ikendelea jana nje kidogo ya mji wa Tarime, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Costanine Massawe alisema hakuwa na habari, kwani taarifa alizokuwa nazo ni kuwa watu wa maeneo hayo wangefanyia tohara nchini Kenya.

"Hizo taarifa kuwa wanafanyia maeneo ya hapa karibu ndiyo unanipatia wewe sasa hivi, taarifa nilizonazo ni kuwa Wakurya wangefanyia maeneo ya Kenya, sasa labda ndiyo
nifanyie kazi taarifa zako...unajua hili suala kwa kweli sasa limepungua tofauti na huko nyuma."

No comments:

Post a Comment