07 November 2013

MBUNGE CHADEMA AWEKWA RUMANDE



 Na Jovither Kaijage,
  Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kwa tiketi ya CHADEMA, Salvatory Machemli, amefutiwa dhamana mahakama kutokana na wadhamini wake waliokuwa wamemdhamini kukosa sifa, huku yeye akishindwa kuhudhuria mahakamani katika kesi ya uchochezi inayomkabili ilipotajwa
. Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ukerewe, Faustine Kishenyi, baada ya upande wa mashtaka kuomba mshtakiwa afutiwe dhamana. Hakimu aliagiza mbunge huyo apelekwe gerezani siku 14 na baada ya hapo ndipo mambo mengine yaweze kuendelea.
Mbali ya kufutiwa dhamana pia mbunge huyo ametakiwa kuwasilisha vitambulisho vyake kituo cha polisi na hatakiwi kutoka nje ya wilaya hiyo bila kibali cha mahakama.Mahakama imelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya mshtakiwa huyo na wadhamini wake watatu kushindwa kufika mahakamani tarehe ambayo kesi hiyo ilipangwa na mahakama. Akifafanua zaidi, hakimu huyo alisema mbali ya mshtakiwa kutofika mahakamani, pia wadhamini wake watatu wamepoteza sifa, hivyo udhamini wao umefutwa.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi Inspekta, Samweli Onyango, alisema mshtakiwa kwa makusudi amekuwa akishindwa kufika mahakamani zaidi ya mara tano bila kutoa taarifa wakati kesi yake ikitajwa.
Mwishoni mwa mwezi uliopita hakimu alimwamuru mmoja wa wadhamini wake, Max Mhogo, awekwe rumande kwa siku saba tangu Oktoba 23 hadi 30 mwaka huu, alitakiwa kufika mahakamani hapo jana na mshtakiwa pamoja na wadhamini wenzake. Mhongo alitekeleza amri hiyo ya mahakama
  Katika utetezi wake Machemli kuhusiana na sababu za kutohudhuria kesi, alisema ameshindwa kufika mahakamani kama ilivyopangwa kwa sababu ya tarehe ya kesi yake kuangukia ratiba za vikao vya Bunge.
Katika kesi yake jana mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri ambao ni aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ukerewe, Japhet Lusingu na Koplo Juma walitoa ushahidi wao.
  Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 20, mwaka huu ambapo mashahidi wengine watatu wa upande wa Jamhuri wataendelea kutoa ushahidi wao. Habari ambazo gazeti hili lilipata wakati linaenda mtamboni zinaeleza kuwa juhudi za kumwekea dhamana mbunge huyo zilikwama kutokana na wadhamini wake kushindwa kuwasilisha hati ya nyumba na badala yake kutoa mali kauli.

2 comments:

  1. Mhe. Lissu kamsaidien Mheshimiwa Machemli. Naona Hakimu ana hasira nae katumwa nini?

    ReplyDelete
  2. Sasa ni wakati wa kuchagua mbichi na mbivu ndani ya chadema. Mkitaka tuwaunge mkono toeni hao mabaunsa wenu kwanza.

    Kila mtu katumwa! Nyie mmetumwa na nani kukashfu na kudharau kila kila kitu?

    Chadema mnaabisha sana na tumewachoka na oparesheni zenu za fujo, matusi na dharau.

    ReplyDelete