Na Rachel Balama
Wadau wa habari hapa nchini wameazimia
kusitisha kuandika , kutangaza na kupiga picha shughuli zozote
zitakazowahusisha au kuratibiwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dkt. Fennella Mukangara na Msemaji wa Serikali Assah Mwambene hadi
hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, wadau hao walitoa tamko hilo
jijini Dar es Salaam
jana wakati walipokutana kujadili mwendelezo wa Serikali wa kufungia vyombo vya
habari.
Wadau hao walisema kuwa,
adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia jana na kuongeza kwamba wataendelea
kupinga Sheria ya Magazeti ya mwaka 1979 kwa kupigia kelele kufutwa kwa sheria
hiyo.
Walisema, pia wataongeza
nguvu ya kisheria mahakamani kwenye kesi iliyofunguliwa na kampuni ya Hali
halisi Publishers Ltd, mwaka 2009 inayopinga sheria hiyo ambapo waliwaomba
wananchi wawaelewe kwa kuchukua hatua hiyo.
Pia wadau hao walidai wamesikitishwa na hatua ya Serikali ya
kutosikiliza kilio cha wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi,
taasisi za vyombo vya habari, wasambazaji wa magazeti na watu wengine wa
kawaida juu ya kuyaondolea adhabu magazeti matatu ya Mwanahalisi, Mtanzania na
Mwananchi yaliyofungiwa na Serikali.
"Aidha, wadau wamesikitishwa
na hatua ya Serikali ya kupuuza kilio chao cha kuomba kusitishwa kwa Sheria
Kandamizi ya Magazeti ya mwaka 1976 na kudhoofisha mchakato wa kuibadilisha
sheria hiyo iliyotajwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992 kuwa ipo
kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," ilieleza taarifa
hiyo.
Uamuzi huo
ulifikiwa na wadau hao kutoka Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari (MOAT),
Jukwaa la Wahariri (TEF), MISA Tan, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa
Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Dar City Press Club (DCPC) na
Tanzania Human Rights Defenders (THRDC)..
No comments:
Post a Comment