Na Alex Marwa
Hivi karibuni viongozi mbalimbali wa Chama na serikali wamekaririwa
wakitoa kauli zenye mkanganyiko na maamuzi mbalimbali ambayo yameacha
sintofahamu kwa wananchi.Kiongozi mzuri
ni yule anayeheshimu utawala wa sheria na hivyo kuzingatia taratibu na sheria
zilizowekwa ambazo yeye ana wajibu wa kuzisimamia wakati wa kutoa maamuzi
mbalimbali, hususan yanayowagusa wananchi moja kwa moja.
Zipo kauli
tata ambazo zimewahi kutolewa na viongozi mbalimbali, ikiwamo ile ya kila mtu
atauchukua mzigo wake mwenyewe, wakikaidi amri halali wapigwe tu, ikibidi kula
nyasi mtakula lakini ndege ya Rais lazima inunuliwe, hivi ni vijisenti tu,
asiyeweza kulipa nauli mpya kigamboni apige mbizi ndiyo nilitumia helikopta ya
jeshi kwenda nayo kwetu Urambo Mlitaka nipande punda?
Kauli tata
nyingine ni wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wanafikiria kwa kutumia makalio,
foleni Dar es Salaam ni ishara ya maisha bora, mnauliza mvua kwani mimi ni
waziri wa mvua, acheni wivu wa kike na wapo walioenda mbali zaidi na kutoa
lugha chafu wakati vikao vya bunge vikiendelea huku wakionekana moja kwa moja
kwenye runinga.
Kwa siku
kadhaa zilizopita mpaka sasa nimekuwa nikafuatilia kwa karibu matukio
mbalimbali yanayojiri katika ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw. Abdallah Bulembo, anayoifanya katika wilaya zote
za Mkoa wa Tanga.
Miongoni mwa
yaliyojiri katika ziara ya Mwenyekiti huyu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama
Cha Mapinduzi; ni agizo lake la kuwarudisha nyumbani wanafunzi 21 wakiwemo wa
kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Kideleko, iliyopo wilayani Handeni kwa
kushindwa kulipa ada.
Ambapo
alikaririwa akisema "huwezi kufuta sifuri kama
wanafunzi wanaenda shule na kushindwa kulipa ada, kwani ada hiyo ndiyo
inawezesha shule kujiendesha, hivyo wanafunzi wote wanaodaiwa warudi nyumbani
hdi watakapopata ada."
Aidha, Bw.
Bulembo aliahidi shilingi laki 5 kwa kila mwanafunzi wa shule za Jumuiya ya
Wazazi atakayemaliza kidato cha nne na kupata daraja la kwanza; na kuwaagiza
wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kwemvumo,iliyopo kata ya Mponde, tarafa ya
Soni wilayani Lushoto, waandamane hadi ofisini kwa mkuu wa shule iwapo dakika
tano zitapita mwalimu hajaingia darasani.
Na kusisitiza
kuwa kuanzia mwakani ada ya shule za Jumuiya ya Wazazi zitapanda kutoka viwango
vya sasa shilingi 650,000 hadi shilingi milioni 1.2 (bweni) na shilingi 350,000
hadi shilingi 600,000 (kutwa) na lengo likiwa ni kufuta daraja la sifuri,
ambapo yeye anaamini kwa kuongeza ada ufaulu utaongezeka, jambo ambalo huenda
likawa na mada pana tukizitazama shule za kata ambazo ada yake ni ya bei nafuu.
Wakati
akiendelea na ziara yake, mwanzoni mwa wiki hii Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya
Wazazi Taifa ya Chama Cha mapinduzi akihutubia mkutano wa hadhara kata ya Duge,
wilayani Tanga amekaririwa na vyombo vya habari akimtaka Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, aache kukurupuka na
kuingilia uhuru wa wananchi kutoa maoni ya katiba na kusisitiza kuwa msimamo wa
Chama Cha Mapinduzi ni serikali mbili.
Hali hiyo
ilipelekea Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia kwa mwenyekiti wake, kujibu
shutuma hizo kwa kuwataka wanasiasa kujadili rasimu iliyotolewa badala ya
kuhangaika na tume au wajumbe wake.
Aidha, Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye naye alilazimika
kutoa ufafanuzi ya kwamba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama Cha
Mapinduzi Abdallah Bulembo hakutumwa na CCM kuishambulia na kuishutumu Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na Jaji Warioba kwa kuwa si msemaji wa chama hicho na
kuitaka jamii na Tume hiyo ielewe kwamba hayo yalikuwa ni mawazo yake binafsi.
Mbali na baadhi ya
matukio niliyoyataja hapo awali, nimelazimika kuchukua kalamu na kuandika
makala haya baada ya kusoma gazeti la Majira toleo namba 7210 la
Jumatano Oktoba 2, 2013 na kuguswa habari iliyobebwa na kichwa cha habari
kinachosema "Bulembo afukuza mwalimu."
Nilivutiwa na habari hii na kutaka kufahamu
kwa undani nini hasa kilichojiri na kupelekea mwalimu huyu kufukuzwa kazi.Akiendelea
na ziara yake mkoani Tanga, Bw. Bulembo alitoa agizo kwa Mkuu wa Shule ya
Sekondari Boza iliyopo wilayani Pangani,mkoani Tanga Bw.Gideon Masue kumfukuza
kazi Mwalimu Salmini Mmari kwa kile alichodai mwalimu huyo kukosa busara,
ustaarabu na kujaa dharau, baada ya kukataa kutaja kiwango chake cha mshahara
mbele ya Bodi ya shule,walimu na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa
na wilaya waliokuwepo ukumbini.
Kimsingi hata kama Shule ya Sekondari Boza
inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo Bw. Bulembo
ndiye Mwenyekiti wake, bado mwalimu Salmin Mmari ilikuwa sahihi kwa kukataa
kutaja kiwango cha mshahara wake hadharani na Bw. Bulembo hana mamlaka ya
kumlazimisha afanye hivyo.
Aidha, uongozi wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya
Chama Cha Mapinduzi na bodi ya Shule ya Sekondari Boza kwa ujumla wao hawana
mamlaka ya kutaja hadharani mshahara wa mwalimu huyo kwa mujibu wa Sheria ya
kazi ya mwaka 2004, kifungu cha 70, kifungu kidogo (2)(d) kinachozuia mwajiri kutoa
taarifa binafsi za mwajiriwa bila ya ridhaa yake.
Jumuiya ya Wazazi kama
mwajiri inaweza kutangaza viwango vya mishahara vya walimu wanaofundisha katika
shule zake kwa ujumla wake, lakini si kwa mwalimu mmoja mmoja mathalan kutaja
hadharani kuwa mwalimu Mmari mshahara wake na marupurupu mengine ni kiasi
fulani.
Sheria ya Kazi kifungu cha 27 kifungu kidogo
(1)(c) kimeainisha wazi kuwa malipo ya mshahara iwapo yanafanyika kwa fedha
taslimu au hundi, yalipwe kwenye bahasha iliyofungwa, na hii inadhihirisha wazi
kuwa mshahara wa mtu ni siri kati ya mwajiri na mwajiriwa.
Mwajiriwa ni tofauti na kibarua, kwa kuwa kwa
upande wa vibarua inajulikana wazi kuwa kwa kutwa wanalipwa kiasi fulani, hivyo
hata ukiwapanga foleni na kumpa kila mtu hela yake mkononi si tatizo, lakini
tunapokuja kwa upande wa mwajiriwa hali ni tofauti na ndio maana Sheria
inamtaka mwajiri kutoa malipo kwa staha, ikiwemo fedha taslimu na mchanganuo
wake ndani ya bahasha iliyofungwa, hundi na mchanganuo wake, au mchanganuo
'bank slip' uliofungwa kama fedha hizo zimewekwa katika akaunti ya mwajiriwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa
Chama Cha Mapinduzi ameonyesha udhaifu mkubwa katika mambo mawili, mosi kitendo
cha kumtaka Mwalimu Mmari ataje mshahara wake hadharani hakikuwa sahihi na
naungana na mwalimu huyo kwa ujasiri aliounyesha wa kukataa kufanya hivyo.
Pili kitendo cha kumfukuza kazi mwalimu
'kiholela' bila ya kufuata utaratibu si cha kiungwana, kwa mujibu wa sheria za
kazi; yapo makosa ambayo yanaweza kusababisha mtu afukuzwe kazi lakini si hili
la kumtaka mtu bila ya ridhaa yake atoe taarifa zake binafs; na mbaya zaidi
Mwalimu Mmari hakupewa muda wa kujitetea.
Mwalimu Mmari ambaye kwa mujibu wa maelezo
yake amefundisha shule hiyo kwa miaka 13 mfululizo hakutendewa haki; na hii
inadhihirisha ni jinsi gani mchango wa walimu hauthaminiwi, mtu ambaye
amejitolea miaka 13 anafukuzwa kazi kwa kudhalilishwa, cha kushangaza mpaka
sasa sijasikia tamko lolote kutoka kwa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wala
kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kuhusiana na uonevu huu.
Mbali na kusikia mwalimu huyu akikaririwa
akisema kuwa anajutia kitendo chake cha kukataa kutaja mshahara wake, kwani
hakujua kama anakosea kwa kuwa anaamini mshahara ni siri kati ya mwajiri na
mwajiriwa, na kama akipata nafasi ya kujitetea
atafanya hivyo.
Naamini Chama Cha Walimu Tanzania (CWT)
kinawajibika moja kwa moja katika kumtetea mwalimu huyu, ambaye pamoja na
utumishi wake kwa kipindi cha miaka 13 lakini bado mchango wake haukuthaminiwa
na hii itawavunja moyo walimu wengine, ambao wengi wao wanafanya kazi katika
mazingira magumu ikiwemo ukosefu wa nyumba za kuishi, uhaba wa vitendeakazi,
kipato duni, hali kadhalika kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi.
Viongozi ni kioo cha jamii na hivyo wanapaswa
kuchukua tahadhari kabla ya kutoa kauli, maamuzi hadharani, kwa kuwa huenda
wananchi wakatafsiri isivyo na hii ikapelekea chuki katika ya wananchi na
viongozi, hivyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi bado ana nafasi ya kutafakari
kauli zake na uamuzi wake wa kutoa agizo la kumfukuza kazi mwalimu huyu kabla
hajachelewa.
Aidha,
kiongozi anapoamua kutoa maoni yake kuhusiana na jambo lolote kama vile Katiba
Mpya, ni muhimu akaweka wazi kuwa anachofanya ni kutoa maoni yake binafsi na si
maoni ya jumuiya au chama, kwa kuwa naamini hata wanachama wa Jumuiya au vyama
wana haki ya kutoa maoni yao
binafsi, kwani hiyo ndio demokrasia ya kweli
No comments:
Post a Comment