Gari yenye namba STK 3665 likiwa ndani ya kiwanda kimoja kilichopo Mbagala, Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) ambapo dereva wake alikamatwa akidaiwa kutaka kumtapeli mmiliki wa kiwanda hicho ambaye ni mteja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) juzi jioni.
Na
Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi mkoani Temeke, linamshikilia dereva wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliyefahamika kwa jina la Bw. Samwel
Mulagalazi, ambaye anadaiwa kushirikiana na watu wawili waliotaka kumtapeli
mteja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), sh. milioni 60
Tukio hilo limetokea juzi saa 11 jioni katika kiwanda kilichopo
Mbagala, Dar es Salaam
(jina tunalo), ambapo matapeli (vishoka), waliojifanya wafanyakazi wa TANESCO,
Makao Makuu, Ubungo, walitaka kufanya utapeli huo kwa mmiliki wa kiwanda hicho.
Matapeli hao
walimpigia simu mmiliki wa kiwanda hicho (jina tunalo), wakidai kiwanda chake
kinaiba umeme hivyo walimtaka atoe sh. milioni 60 asiweze kukatiwa umeme.
Mmiliki huyo
akitambua kuwa mita zake hazikuwa na tatizo lolote na hahusiki na wizi huo,
aliwasiliana na Meneja wa TANESCO wilayani Temeke, Mhandisi Richard Mallamia na
kumweleza vitisho alivyopewa na matapeli hao na pesa waliyotaka kupewa.
Mhandisi Mallamia alimtaka mteja huyo wa
TANESCO, kutowakatisha tamaa matapeli hao badala yake awapigie simu ili waende
kuchukua pesa hizo.
Baada ya kumpa ushauri huo, Mhandisi Mallamia
alifanya mawasiliano na ofisi ya shirika hilo
Idara ya Usalama na Jeshi la Polisi mkoani Temeke ili wakaweke mtego.
Akizungumza na Majira, Mhandisi Mallamia
alisema baada ya matapeli hao kupigiwa simu ili waende kuchukua pesa
walizotaka, awali walikubali lakini baadaye walimpigia simu mteja wao na kudai
wanamtuma dereva.
Bw. Mulagalazi alifika kiwandani hapo kama dereva aliyetumwa na matapeli hao akiwa na gari Land
Cruiser Hardtop, yenye namba SKT 3665 na kuingia mtegoni (kukamatwa).
Maofisa wa TANESCO na polisi walimtaka
mmiliki wa kiwanda awapigie simu matapeli hao na kuwajulisha tayari ametoa pesa
hizo kwa dereva wao. Vishoka hao walimpigia simu dereva na kumtaka wakutane
maeneo ya Mbagala.
Polisi na Maofisa wa TANESCO waliingia ndani
ya STK ambalo lilikuwa l ikiendeshwa na mtuhumiwa ili kwenda kuwakamata
matapeli hao ambao walipaki gari lao barabarani.
Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa,
matapeli hao wakiwa na gari aina ya RAV 4, waliiona STK ikiwafuata taratibu
bila kujua ndani ya gari kulikuwa na Maofisa wa TANESCO na polisi ambao
walijificha ili wasionekane.
Dereva (mtuhumiwa), alisimama, kushuka kwenye
gari na kuwafuata matapeli hao akiwaambia TANESCO wamechukua kitambulisho chake
hivyo matapeli waliingia kwenye gari na kukimbia kwa mwendo wa kasi.
Mtuhumiwa (dereva), alirudi katika gari na
polisi walimtaka warudi Kituo cha Polisi Mbagala. Hadi jana mchana bado alikuwa
akiendelea kuhojiwa.
Inadaiwa kuwa, katika
maelezo yake dereva huyo ambaye inadaiwa anamuendesha Mratibu wa Mradi wa
Kibamba, aliwataja watu waliomtuma kwa majina ya Godfrey Mjakamaarufu 'Makofia'
na Modest Kayombo Thomas.
Alidai Thomas ni mwanafunzi wa Chuo cha
Teknolojia Dar es Salaam
(DIT) ambaye amejenga maeneo ya Vikindu na Mjaka ni fundi umeme ambaye hupata
tenda mbalimbali.
Katika utetezi wake baada ya kukamatwa,
inadaiwa mtuhumiwa alidai yeye hakuwa akifahamu lolote zaidi ya kuambiwa
akachukue mzigo ambao hakujua ni mzigo gani.
Taarifa za uhakika zinasema kuwa, vishoka hao
Mjaka na Thomas wana kesi Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, ambayo inaendelea
kusikilizwa na itatajwa Oktoba 15 mwaka huu, wakidaiwa kujifanya wafanyakazi wa
TANESCO na walikamatwa wakiwa wamevaa sare za shirika hilo.
Chanzo hicho kilidai watu hao walikamatwa
wakifanya utapeli kwa wateja wa TANESCO eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.Kamanda
wa Polisi mkoani humo, Engelbert Kiondo, alisema tukio hilo atalitolea ufafanuzi leo baada ya kupata
taarifa kamili.
Mhandisi Mallamia alisema kukamatwa kwa
mtuhumiwa ni matokeo ya elimu wanayoendelea kuitoa kwa wateja wao ambao
wanatumia umeme mkubwa wakiwemo wamiliki wa viwanda, bekari za mikati, hoteli
pamoja na wateja wadogo ili wawe makini kujiepusha na matapeli wa aina hiyo.
Alisema hivi sasa kuna
mtandao mkubwa ambao unalihujumu shirika hilo
kupitia wateja wake na kuchafua sifa ya TANESCO kwenye jamii jambo ambalo
haliwezi kuvumilika.
No comments:
Post a Comment