WASHINGTON,
Marekani
Nchi ya Marekani
imelazimika kufunga baadhi ya shughuli za Serikali kuanzia jana, baada ya Bunge
la nchi hiyo kuikataa bajeti yake wakipinga mabadiliko ya kisheria yanayohusu
sekta ya afya yaliyofanyika hivi karibuni.
Idadi kubwa ya
watumishi wa Serikali watakosa ajira ambapo idara nyingi za Serikali zimeambiwa
zifunge milango wakati matumaini ya suluhisho la mtafaruku huo wa bajeti ambao
unahusisha wabunge wa chama tawala cha Democrat dhidi ya Republicans yakizidi
kufifia.
Wataalamu
mbalimbali nchini humo walidai kuwa, uamuzi wa kusitisha huduma zisizo muhimu,
utaathiri uchumi wa nchi hiyo kwa kiwango kikubwa.Wafanyakazi
katika vitengo mbalimbali vya Serikali, jana alfajiri walijikuta wakirudishwa
majumbani karibu 800,000 kati yao
wakiambiwa wachukue likizo bila malipo hadi mwafaka utakapopatikana.
Marekani
imesema wafanyakazi ambao watabakizwa kazini ni wale ambao shughuli zao
haziwezi kusimama kama madaktari, manesi,
waongoza ndege na wafanyakazi wa Shirika la Posta nchini humo.Kwa mujibu wa
Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), ilisema baadhi ya huduma za umma kama miradi ya utafiti wa tiba zinazoendeshwa na idara za
Serikali zitasimama.
NASA ambacho
ni kitengo kinachofanya tathmini za usafiri wa kwenda sayari nyingine na anga
za mbali, wafanyakazi asilimia 95 wamepewa likizo bila malipo katika kipindi
hiki.Marekani
imefikia hatua hiyo baada ya Baraza la Seneti linalodhibitiwa na Chama cha
Democrat kukataa pendekezo la wajumbe wa Chama cha Republican la kuusimamisha mpango
wa huduma za afya wa Rais Obama ujulikanao kama
Obama Care.
Wabunge wa Republican
wanaolidhibiti Baraza la Wawakilishi, walikuwa tayari kuipitisha bajeti hiyo
kwa sharti la kuusimamisha mpango wa afya wa Obama ambao umeanza kutekelezwa
jana.Kutokana na kufungwa
kwa shughuli za Serikali, Rais Barack Obama wa nchi hiyo alisema; "Kwa
bahati mbaya Bunge halikutimiza wajibu wake".
Rais Obama aliwatumia
wanajeshi ujumbe wa video akisema; "Kama
amiri jeshi wenu, nimehakikisha kwamba mtaendelea kuwa na uwezo, zana na yote
mnayoyahitaji ili kuutekeleza wajibu wenu kwa Taifa."Vitisho kwa
Taifa letu, bado havijabadilika hivyo tunawataka muwe tayari kwa dharura
yoyote," alisema Rais Obama na kuwashukuru askari wa kujitolea na wale wa
Idara ya Ulinzi kwa huduma zao."
Kila upande unaulaumu
mwingine kushindwa kufikia makubaliano ambapo Rais Obama amehadharisha madhara
ya kiuchumi yanayoweza kutokea kutokana na kusimamishwa shughuli za Serikali
akisema kasi ya ustawi wa uchumi inaweza kuvurugika.
Hatua iliyofikiwa
jana pia imesababisha wasiwasi kama Marekani itafikia lengo lake hadi
katikati ya Oktoba mwaka huu la kuongeza deni la Serikali hadi dola trilioni
16.7.
Hisa barani Ulaya
zimepanda mapema jana ambapo wawekezaji vitega uchumi wameingiwa wasiwasi. Wachunguzi
wanaamini kuwa, wabunge wa Marekani watakaa chini haraka ili kutafuta ufumbuzi.
Wakati huo huo, uchunguzi wa maoni
umeonesha Chama cha Republican kitalaumiwa na wananchi wengi wa Marekani
kutokana na kufungwa kwa shughuli za Serikali.
No comments:
Post a Comment