Na Amina Athumani
UONGOZI wa Yanga umelalamikia rufaa
waliyoiwasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya
Sheria na Hadhi za wachezaji kuhusu kupinga kufungiwa mchezaji wao, Mrisho
Ngassa bado haijasikilizwa huku muda ukizidi kwenda.
Akizungumza Dar
es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema waliwasilisha
rufaa hiyo tangu Agosti 23, mwaka huu, lakini hadi jana haijasikilizwa na
endapo watashindwa kupewa ufafanuzi kuhusu pingamizi hilo, watafuata hatua na
taratibu stahiki.
Alisema rufaa
waliyoiwasilisha ni kupinga adhabu aliyopewa Ngassa, ambayo wanadai ni ya
uonevu na inakiuka kanuni za mashindano, misingi ya sheria na haki za msingi za
mchezaji wao.
Alisema Yanga
ilipokea barua ya TFF Agosti 16, mwaka huu ikielezea adhabu aliyopewa Ngassa ya
kufungiwa mechi sita na adhabu ya kulipa faini ya sh. milioni 30 na riba ya
asilimia 50 ya sh. milioni 15 ambazo zinafikia jumla ya sh. milioni 45, huku
wakishindwa kutaja kifungu cha kanuni aliyokiuka mchezaji wao.
"Yanga inaiona adhabu hii kuwa ni
ya uonevu, kwa klabu na mchezaji inayokiuka kanuni za mashindano hayo, misingi
ya sheria na haki za msingi za mlalamikiwa," alisema Mwalusako.Alisema sababu za Yanga kuwasilisha
rufaa yao na kupinga adhabu hiyo TFF ni kamati kukosea kanuni na sheria ya
kumuadhibu Ngassa kwa kuzingatia mkataba batili uliowasilishwa na Simba.
"Suala la usajili wa mchezaji
Ngassa, baina yake na Simba mara baada ya msimu wa 2012/2013 kumalizika ulikuwa
na matukio makubwa yaliyomhusu Ngassa, Klabu ya Simba na Klabu ya Azam."Kamati ya sheria na hadhi za
wachezaji ya TFF ilipaswa kuyarejea, kabla ya kufikia uamuzi waliofikia hasa
kwa kuzingatia mchezaji hakuwepo kujitetea katika kikao hicho," alisema
Mwalusako.
Alisema pia kamati ilikosea kanuni na sheria
kwa kutoa uamuzi kwa ushahidi wa upande mmoja pasipo kumsikiliza Ngassa, pia
ilikosea kumuadhibu kwa kuingia mkataba na Simba nje ya kanuni za usajili.Mwalusako alisema pia pingamizi hilo
linaeleza kuwa kamati hiyo, ilikosea kisheria kwa walioweka pingamizi kuwa
sehemu ya kutoa uamuzi ambapo pia ilikosea kikanuni kuinyima Yanga kumtumia,
Ngassa katika mechi sita pasipo na sababu za msingi.
Alisema kutokana na sababu hizo
anaimani rufaa yao, itasikilizwa na kutendwa haki inayostahiki kwa mchezaji
wao, ikiwa ni pamoja na kumuondolea adhabu ambazo hakustahili mchezaji wao
kupewa.Ngassa
mpaka leo atakuwa amekosa mechi tatu, kati ya sita zilizomo katika adhabu yake
ikiwa ni mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, Ashanti United na Coastal Union
inayotarajiwa kuchezwa leo.
No comments:
Post a Comment