Leah Daudi na Flora Nkya
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia
watuhumiwa wawili, mmoja kati yao ni dereva wa
gari la Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kwa tuhuma za kuiba transfoma ambayo
ni mali ya shirika hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa
Polisi wa kanda hiyo, Kamishna Suleimani Kova, alisema washtakiwa hao
walikamatwa Agosti 16 mwaka huu, saa 6:30 usiku huko, eneo la Ofisi za
TanescoKinondoni.
Alisema watuhumiwa hao walikutwa wakiiba transfoma ambapo polisi
walipata taarifa za wizi huo kutoka kwa Wasamaria wema na kuweka mtego.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Daniel Milanzi (32) na Shukuru
Jemes (33) mkazi wa Buguruni wakiwa wanatumia gari namba SU 37150, aina ya Toyota
Dyna, mali
ya TANESCO waliyokuwa wakiitumia katika wizi huo.
"Gari linashikiliwa polisi kama
kielelezo cha wizi huu, watuhumiwa wanaendelea kushikiliwa kwa mahojiano baada
ya upelelezi kukamilika," alisema.
Kamishna Kova alisema, katika tukio lingine Agosti 13 mwaka huu,
maeneo ya Mbezi Makabe, polisi waliokuwa doria walipata taarifa kutoka kwa Bw.
Evaristi Masambinga aliyedai kuibiwa gari lake na
majambazi wanne ambao waliondoka nalo.
Alisema
baada ya polisi kupata taarifa hizo, walifanya msako mkali na kufanikiwa
kulikamata saa nane usiku likiwa limetelekezwa umbali wa kilomita mbili kutoka
eneo la tukio ambapo polisi wanaendelea kuwasaka majambazi hao.
No comments:
Post a Comment