Na Elizabeth Joseph, Dodoma
CHAMA cha Wasindikaji wa Mafuta ya Alizeti Tanzania (TASUPA)
kimetoa siku kumi na nne kwa mmiliki wa Kiwanda cha Murzah Oil Mills Group of
Companies kukanusha kauli yake aliyoitoa kudai kuwa mafuta ya alizeti hayana
ubora kwa matumizi ya binadamu
. Rai hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na Mwenyekiti wa chama hicho,
Ringo Iringo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na
kuongeza kuwa mmiliki wa kiwanda hicho alitoa kauli ya kudai kuwa mafuta hayo
hayajakidhi viwango na ubora kwa matumizi ya binadamu jambo ambalo halina
ukweli ndani yake na kumtaka kuomba radhi kabla hatua kali za kisheria hazija
chukuliwa dhidi yake.
Iringo alisema kuwa hata wateja wao kwa sasa wameingiwa na
wasiwasi hali inayochangia kukosa soko la uhakika la mafuta hayo jambo
linalosababisha kushuka kwa kipato kwa watengenezaji hao.
"Wasindikaji wa mafuta ya alizeti walipata hasara ya kiasi
cha shilingi bilioni tano huku akitangaza kuwa alizeti ndiyo haina ubora jambo
ambalo tunalipinga vikali kwani hata kiafya inashauriwa kuyatumia mafuta ya
alizeti na tayari yalishathibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na
Shirika la Viwango (TBS)," alisema Iringo.
Hata hivyo alieleza kuwa chama hicho kipo tayari kwenda katika
Tume ya ushindani kwa kushindanishwa ubora wa bidhaa hizo pamoja na kuandaa
wanasheria wao ili kuhakikisha kauli hiyo inafutwa na kusafishwa ili kuondoa
wasiwasi kwa watumiaji wa mafuta hayo.
No comments:
Post a Comment