20 August 2013

MTOTO WA MANGULA ALIZA WENGI



Na Mariam Mziwanda
RAIS Jakaya Kikwete, jana aliongoza mamia ya wananchi kutoa heshima za mwisho kwenye msiba wa Nelema Mangula (25), ambaye amefariki dunia mwishoni mwa wiki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine walioshiriki kutoa heshima zao ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda.

Taratibu za kutoa heshima za mwisho zilifanyika Masaki, Dar es Salaam nyumbani kwa baba mzazi wa marehemu Bw. Philip Mangula ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumzia wasifu wa marehemu, Bw. Mangula, alisema kifo hicho kimezima ndoto ya mtoto wake kuwa rais miaka 20 ijayo ambapo kauli hiyo iliamsha vilio kwa baadhi ya watu waliokwenda kuomboleza msiba huo.
"Marehemu alikuwa na ndoto za kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania lakini ndoto yake imepotea," alisema Bw. Mangula.
Alisema marehemu alipata ajali Agosti 16 mwaka huu, wakiwa katika sherehe za kumuaga mchumba wa kaka yake ambaye ndoa yao ilifungwa Agosti 17 mwaka huu.
Marehemu alikutwa na mauti wakati familia ya Mangula ikiwa kwenye hekaheka ya harusi ya kijana wao Malumbo Mangula, ambapo ndoa hiyo ilifungwa Agosti 17 mwaka huu, saa 10 jioni muda ambao alifariki dunia.
Katika ajali hiyo, ilibainika marehemu amepasuka mishipa ya damu kwa ndani hivyo kuna damu ilikuwa imevilia lakini alifariki dunia wakati madaktari wakitaka kumfanyia upasauji.
Marehemu alizaliwa Septemba 21,1988 akiwa ni mtoto wa mwisho kati ya watoto wanne wa Bw. Mangula.

2 comments:

  1. Natoa pole sana kwa familia ya Mh Philipo Mangula,inasikitisha ina huzinisha kwani siku zote kizuri huwa hakikai Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi amin

    ReplyDelete