23 August 2013

MITAMBO SONGAS YAUNGUA



 BAADHI ya wakazi waishio maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, watakosa umeme kwa muda usiozidi wiki mbili baada ya mitambo ya Songas inayotumika kuzalisha umeme, eneo la Ubungo, Kituo cha 33 KV, kuungua moto jana, anaripoti Salim Nyomolelo.

 Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Bw. Felichism Mramba, alisema moto huo ulianza saa tisa alfajiri na kuteketeza nyaya mbalimbali za mitambo hiyo.Alisema hali hiyo ilisababisha umeme wa gridi ya Taifa Mkoa wa Dar es Salaam, kuzimika kwa muda ambapo kutokana na kuungua kwa nyaya hizo, baadhi ya maeneo yatakosa umeme.
“Maeneo ambayo yatakosa umeme ni Kimara, Chuo Kikuu, Ubungo, Tabata, Mbezi, Kigogo, Mburahati, Magomeni, Tandale, Changanyikeni, Riverside na Buguruni,” alisema Bw. Mramba.Aliongeza kuwa, hadi jana asubuhi chanzo cha moto huo na hasara ilikuwa haijafahamika ambapo kazi ya kufanya tathmini pamoja na matengenezo, yataanza mapema ili kurudisha huduma.
“Nawaomba wakazi wote wa Dar es Salaam, watuwie radhi kutokana na tatizo hili, matengenezo yataanza mapema ili kurudisha umeme katika maeneo yao,” alisema.Alisema wataangalia ukubwa wa tatizo, vifaa vilivyoungua na upatikanaji wake ili kurudisha umeme ambapo maeneo ambayo yameathirika, yanaweza kupewa umeme kutoka katika vituo vingine na taarifa kitatolewa kwa wananchi.
Bw. Mramba alisema vikosi vya Zima Moto na Uokoaji vilifika eneo la tukio mapema na kufanikiwa kuuzima moto huo saa 1:15 asubuhi.Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi, Jesuald Ikonko alisema umeme ulizima saa 9:45 alfajiri na wao kupata taarifa za moto saa 11:58 asubuhi na ilipofika saa 12:05, walifika eneo hilo.

1 comment: