10 January 2013
Wakulima wa mpunga walivyonufaika na pembejeo za kilimo Tabora
Na Baker Kitundu
SERIKALI imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha mkulima anakuwa na maisha bora kupitia kilimo cha kisasa.
Moja ya njia za kuwainua wakulima nchini ni uanzishwaji wa ruzuku ya pembejeo wa mwaka 2008, licha ya watendaji wachache kurudisha nyuma kwa kufanya udanganyifu.
Wakulima wa mpunga katika skimu ya umwagiliaji Mwamapuli Wilayani Igunga, Mkoani Tabora ni moja ya kundi lililonufaika na mpango huo ambapo, wameongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka gunia 15 hadi 55 kwa ekari 1.5 na kuondokana na umaskini.
Mwakilishi wa wakulima 60,000 wa skimu ya umwagiliaji ya Mwamapuli, Helena Mikaeli (36) anasema, pembejeo za kilimo za ruzuku zinazotolewa na MAFC zimesaidia kuboresha uzalishaji wa zao hilo mara tatu zaidi ikilinganishwa na uzalishaji wa awali.
Anaongeza kuwa, ilipoanza mwaka 1991 wakulima walikuwa wakizalisha gunia 15 kwa eneo la 0.6 ya hekari.
"Mwaka 2009 zilipoanza kutolewa pembejeo za kilimo za ruzuku uzalishaji wa mpunga uliongezeka na kufikia gunia 55 kwa eneo la hekta 0.6, pembejeo za kilimo zinazohusika kwenye ruzuku ni pamoja na mbolea za kupandia na kukuzia kwenye zao la mpunga," anasema.
Anasema, ruzuku kwa maana kuwa mkulima hugharamia mfuko mmoja wa mbolea kwa shilingi 26,000 na fedha nyingine ya gharama ya mfuko huo hufidiwa na serikali.
Anasema, bei ya bila ruzuku ya mfuko mmoja wa mbolea ya kupandia hugharimu shilingi 65,000 na mbolea ya kupandia mfuko hugharimu shilingi 45,000.
Akilinganisha gharama za uzalishaji na mapato anasema kuwa, thamani ya gunia 55 yakiuzwa kwa shilingi 60,000 kila moja ni sawa na shillingi 3.3 milioni akaongeza kuwa, kipato hicho ni kikubwa kwani gharama za uzalishaji zinafikia shilingi 600,000 tu na hivyo mkulima kuwa na faida ya shilingi milioni 2.7 ambayo inamtoa mkulima katika umaskini.
"Kipato hicho kimetuwezesha kujijengea nyumba za kisasa, kusomesha watoto kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu. Pia kujinunulia vyombo vya usafiri kama vile baiskeli, pikipiki na magari,"
"Lakini nawaonya wanaume kuacha kutumia chanzo hicho kizuri cha mapato kinachotokana na mauzo ya zao la mpunga kwa kuongeza nyumba ndogo badala yake wafanye mambo ya maendeleo kwa familia zao,"anasema.
Akifafanua utaratibu wa ugawaji pembejeo anasema, kila mkulima wa Kijiji cha Mwamapuli chenye kaya 1,200 zenye jumla ya wakazi 60,000 hupewa mifuko sita ya mbolea ikiwemo mifuko mitatu ya mbolea za kupandia na mifuko mitatu mingine ya mbolea ya kukuzia.
Anasema, mfuko mmoja humgharimu mkulima shilingi 26,000 na fedha nyingine ya gharama ya mfuko huo hufidiwa na serikali. Bei ya bila ya ruzuku ya mfuko mmoja wa mbolea ya kupandia ni shilingi 65,000 na mbolea ya kupandia mfuko shilingi 45,000.
Pamaja na mafanikio hayo anasema, changamoto zinazowakabili ni kutotosheleza kwa pembejeo za ruzuku zinazotolewa kwani hutolewa na kutosheleza eneo la hekari 6,000 wakati eneo linalolimwa ni hekari 13,000.
"Tunaiomba wizara iongeze pembejeo hizo za ruzuku mara mbili ili zitosheleze eneo linalolimwa badala ya kutosheleza eneo dogo kwani wakulima wanajitahidi kutatua changamoto hiyo kwa kujinunulia pembejeo hizo kuongezea kwa hizo zinazotolewa kwa ruzuku."
Pia, ucheleweshwaji kusambazwa pembejeo hususan mbolea ya kupandia kwa wakulima ni changamoto inayowasababishia kuchelewa kupanda msimu wa kilimo na kupunguza uzalishaji.
"Tunaiomba wizara ya kilimo kusambaza pembejeo za ruzuku mapema ili ziweze kutumiwa na wakulima kikamilifu,"anasema.
Mkulima Kayuti Tuba (46), anasema amenufaika na upatikanaji wa mbolea za ruzuku, mafunzo ya kilimo bora cha mpunga na matumizi ya mbegu bora na kuongeza uzalishaji uliompatia kipato na kununua pikipiki.
Anasema, kupitia mafunzo ya kilimo bora cha mpunga yaliyotolewa na Kituo cha Mafunzo cha Moshi (KTC) na kutumia mbegu bora ya mpunga iliyoletwa na Taasisi ya Utafiti kwa Maendeleo ya Kilimo ya Tumbi, (ARI TUMBI) Tabora na upatikanaji wa mbolea za ruzuku na kuzitumia kikamilifu ilimuwezesha kuongeza uzalishaji.
Akieleza kipato alichopata kutokana na mauzo anasema, kila gunia liliuzwa shilingi 60,000 na kujipatia jumla ya shilingi milioni 3.3.
"Kabla ya kuletwa mbegu hii nilikuwa natumia mbegu ya supa ya kienyeji ambayo ilikuwa ikinimpa uzalishaji wa magunia 15 katika eneo la 0.6 ya hekari TXD SARO 306 iliniwezesha na wakulima wenzangu kuzalisha gunia 55 za mpunga katika eneo la 0.6 la hektari," anafafanua Tuba.
Skimu ya Umwagiliaji ya Mwamapuli, wilayani Igunga, ilianzishwa rasmi mwaka 1991. Jumla ya kaya 1,200 zenye jumla ya wakazi 60,000 wanashiriki kwenye skimu hiyo.
Eneo la mradi lina ukubwa wa hekari 13,000 lakini ni eneo la hektari 6,000 tu ndilo linalopata huduma ya pembejeo za ruzuku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment