10 January 2013

Mchango asasi za kiraia nchini unatakiwa kuthaminiwa



Na Suleiman Abeid

TANGU kuanzishwa kwa vikundi vya kijamii nchini maarufu kama Asasi za kiraia ama kwa lugha ya kigeni 'Non Governmental Organization' (NGO's) kumekuwepo na mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali zinazoendeshwa na asasi hizo.


Mbali ya mafanikio hayo pia Watanzania wengi wamekuwa wakinufaika na uwepo wa asasi hizo kupitia mafunzo wanayopatiwa na misaada inayotolewa katika nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya kielimu, kiafya, kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mchango wa asasi za kiraia pia umekuwa ukionekana katika matukio makubwa ya kitaifa ambapo hushirikiana na serikali katika kuihamasisha jamii ili iweze kushiriki kikamilifu matukio mbalimbali kwa mfano mchakato unaoendelea hivi sasa wa ukusanyaji wa maoni juu ya uandikaji wa katiba mpya nchini.

Pia tumekuwa tukiona michango ya asasi hizo katika utoaji wa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kujikinga na maambukizo ya virusi vya UKIMWI na kujiepusha na unyanyapaa kwa watu walioathirika na ugonjwa huo kupitia semina, warsha na makongamano mbalimbali.

Mwaka jana Taifa lilikuwa na zoezi muhimu la Sensa ya Watu na Makazi nchini, tuliona michango ya asasi mbalimbali katika uhamasishaji ambapo asasi zilishiriki kwa njia moja ama nyingine katika kuwahimiza wananchi juu ya umuhimu wa wao kuhesabiwa.

Hata hivyo pamoja na mchango mkubwa katika kusaidiana na serikali kusukuma gurudumu la maendeleo bado wapo baadhi ya Watanzania na viongozi wachache wa serikali wasiothamini michango inayotolewa na asasi hizo huku wengine wakizilinganisha na vyama vya upinzani.

Viongozi hao hasa walioko katika ngazi ya maamuzi katika wilaya wamekuwa kikwazo kimojawapo cha mafanikio ya shughuli zinazoendeshwa na asasi za kiraia ambapo wengine hudiriki kutaka kuzidhibiti kwa kuziweka mikononi mwao huku wakizielekeza nini cha kufanya kwa kuzingatia matakwa yao binafsi.

Hivi sasa Taifa letu lipo katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya katiba mpya ambayo imepigiwa kelele kwa kipindi kirefu hivyo iwapo ratiba itaenda kama ilivyopangwa katiba hiyo mpya inaweza ikaanza kutumika rasmi mwaka 2015 na kuandika historia mpya katika nchi yetu.

Pamoja na Rais Jakaya Kikwete kuruhusu kuandikwa kwa katiba mpya na kutungwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba sura ya 83, lakini bado ulikuwepo umuhimu wa jamii kuelimishwa juu ya umuhimu wa ushiriki wao katika kuchangia maoni ya kitu gani wanahitaji kiingizwe ndani ya katiba hiyo sambamba na kuielewa sheria yenyewe.

Kazi ya kuihamasisha jamii iweze kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa utoaji wa maoni yao juu ya katiba mpya isingekuwa rahisi kazi hiyo kufanywa na serikali peke yake hivyo kuwepo na hitajiko la msaada wa taasisi nyingine katika kufanya kazi hiyo ya uhamasishaji zikiwemo asasi za kiraia.

Hata hivyo kama nilivyoeleza hapo awali baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa wilaya katika maeneo mengi wamekuwa kikwazo kikubwa cha wananchi kuweza kunufaika na elimu inayotolewa na asasi hizo za kiraia zinazojitolea kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi waweze kutoa maoni yao bila ya woga wowote.

Moja ya asasi zilizoonja makali ya viongozi wa aina hiyo ni Mtandao wa Azaki Wilayani Meatu Mkoani Simiyu (MENGONET) ambayo imekuwa ikiendesha zoezi la utoaji elimu ya uraia kwa jamii pamoja na kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kuchangia maoni yao katika katiba mpya ijayo.

MENGONET katika juhudi zake za kutaka kusaidiana na serikali juu ya utoaji wa elimu ya uraia kwa wananchi iliomba ufadhili kutoka Shirika la The Foundation For Civil Society lenye makazi yake jijini Dar es Salaam ambapo baada ya kupata fedha iliandaa ratiba kwa ajili ya uendeshaji wa midahalo katika maeneo mbalimbali wilayani Meatu.

Akizungumzia hali hiyo Mwenyekiti wa MENGONET, Esther Joseph anasema Azaki yake baada ya kupata fedha hizo iliandaa ratiba ya kuendesha midahalo mbalimbali wilayani Meatu midahalo ambayo inalenga  kuimarisha uhusiano wa wananchi, madiwani na wabunge.

Pia anasema mbali ya shughuli za kuimarisha uhusiano lakini pia walikuwa wamepata kibali kutoka Tume ya Mabadiliko ya katiba nchini ili kuwawezesha wananchi watakaoshiriki midahalo hiyo pia waweze kutoa maoni yao juu ya mambo gani wanayohitaji yawemo katika katiba mpya na kisha MENGONET iyatume katika Tume.

Hata hivyo anasema hivi karibuni mkuu wa wilaya ya Meatu Rosemary Kirigini alidiriki kuwazuia kuendesha midahalo katika miji ya Mwandoya na Mwanhuzi wilayani Meatu kwa sababu ambazo hazikuwa za msingi ambapo walipompatia taarifa ya kutaka kuendesha midahalo hiyo aliwakataza akidai yeye binafsi alikuwa nje ya wilaya.

"Tulisikitishwa na hatua hii ya mkuu wetu wa wilaya, hata pale tulipojaribu kumshauri aturuhusu tuendelee na midahalo pamoja na kutokuwepo kwake kwa vile ofisi yake ilikuwa na mwakilishi wake, aligoma kwa madai haruhusu kufanyika kwa mdahalo wowote bila ya yeye kuwepo katika wilaya yake,"

"Lakini pia alitutaka kabla ya kuendesha midahalo hiyo tumwandalie mambo yote ambayo tumepanga kuyazungumza ili aweze kuyahariri kwa madai kwamba mara nyingi asasi zetu zimekuwa zikilenga kuwapoteza wananchi na alitishia kutuweka ndani iwapo tungekaidi amri yake, hivyo ilibidi tubadili ratiba zetu," anasema.

Mwenyekiti huyo anasema kitendo kilichofanywa na mkuu huyo wa wilaya ni wazi kilipingana na sheria ya mabadiliko ya katiba  na kwamba MENGONET ikiwa ni Taasisi inayotambulika kisheria ilichopaswa kufanya ni kutoa taarifa kwa mkuu huyo au kwa mkurugenzi wa wilaya.

"Zuio hili la mkuu wa wilaya linaonesha jinsi gani baadhi ya viongozi wetu wa serikali wasivyothamini michango ya asasi za kiraia hapa nchini, maana hata sheria yenyewe ya mabadiliko ya katiba haikuweka vikwazo vingi kwa watu wanaotaka kuendesha midahalo juu ya utoaji wa maoni ya katiba mpya,"

"Ukiangalia kifungu cha 17 (2) (a) pametajwa orodha ya watu wanaopaswa kupewa taarifa sambamba na vitu vinavyotakiwa kuambatanishwa wakati wa utoaji wa taarifa hiyo ambapo kwa taasisi, jumuiya au kikundi cha watu yapo mambo kadhaa ya kufanya yameelekezwa, ambayo na sisi tuliyatimiza," anasema Bi. Joseph.

Ndani ya sheria hiyo inaelezwa kuwa; "Sheria inataka mtu binafsi, taasisi, jumuiya au kikundi chochote cha watu wenye malengo yanayofanana kutoa taarifa kwa maandishi kwa Tume au kwa niaba yake kupitia Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Serikali ya Mitaa, Mkurugenzi wa Manispaa, Katibu wa Baraza la Mji au Wilaya."

"Sharti la kutoa taarifa ya kuendesha programu ya elimu ya umma kupitia mkuu wa wilaya, mkurugenzi wa serikali za mitaa au mkurugenzi wa manispaa, Katibu wa Baraza la Mji au wilaya hakutakuwa ni sababu ya kuzuiliwa mtoa taarifa isipokuwa kwa sababu zitakazoelezwa wazi kwa mtoa taarifa na Tume kuarifiwa."

Kwa hali hiyo ni wazi kwamba, hata kama mkuu wa wilaya asingekuwepo katika wilaya yake lakini bado palikuwepo na watu wengine wanaoruhusiwa na Sheria hiyo kupewa taarifa na kuruhusu kufanyika kwa shughuli iliyotolewa taarifa na kama pana sababu za kuzuiwa lazima wahusika waelezwe wazi.

Hata hivyo Bi. Joseph anasema MENGONET haikupenda kuvutana na mkuu huyo wa wilaya ambapo walisubiri mpaka pale aliporudi na walipowasiliana naye aliwaruhusu kuendelea na midahalo hiyo iliyofanyika katika kata za Mwandoya na Mwanhuzi mjini hata hivyo hakuweza kuhudhuria wala kutuma mwakilishi wake.

Katika midahalo hiyo ambayo pia ilitumika katika kujadili na kuimarisha uhusiano wa wananchi, madiwani na wabunge wananchi walipata fursa ya kuelezea hali ya mahusiano yao na wawakilishi wao na kutoa maoni yao ya nini kiandikwe katika katiba mpya ijayo.

Katika kata ya Mwandoya, wakazi wa kata hiyo wamependekeza ili kuondoa tabia ya baadhi ya madiwani na wabunge kutoa ahadi za uongo katika vipindi vya kampeni za uchaguzi mkuu nchini ni muhimu katiba ijayo ikaweka kipengele kitakachowalazimisha wagombea kufunga mikataba na wapiga kura wao.

Wananchi hao wamesema mikataba itakayofungwa na wawakilishi hao ieleze wazi ni mambo gani ambayo watawatekelezea wananchi katika kipindi chao cha uongozi cha miaka mitano na kwamba iwapo watakwenda kinyume na mikataba hiyo basi waondolewe katika uongozi bila kusubiri kukamilika kwa muda wao wa miaka mitano.

Kwa upande wake Samson Mbega anasema, "Uzoefu unaonesha kwamba hawa wawakilishi mara baada ya kuchaguliwa wanatusahau sisi wapiga kura wao, naona ni vizuri sasa tukafunga nao mikataba, lakini pia katiba ijayo iruhusu kuundwa kwa chombo maalum kitakachokuwa kikifuatilia utekelezaji wa ahadi zao."

Kwa upande wake mwezeshaji katika midahalo hiyo ya Mwandoya na Mwanhuzi, Obeid Mkina kutoka Jukwaa la Katiba nchini anasema ili wananchi waweze kupata maendeleo ya uhakika katika maeneo yao ni muhimu wakahakikisha wanachagua viongozi wenye moyo wa kuwatumikia badala ya wale wanaotanguliza mbele maslahi yao binafsi.

Anasema uzoefu unaonesha kwamba wananchi wengi kinapofika kipindi cha uchaguzi wamekuwa wakipiga kura bila ya kuzingatia thamani ya kura zao hali ambayo huchangia mara nyingi viongozi wanaochaguliwa kutowajibika zaidi kwa wapiga kura hao.

"Wananchi mnapaswa kuelewa maana ya kura mnazozipiga katika chaguzi mbalimbali za kuwachagua viongozi wetu, eleweni kura zenu zina thamani kubwa katika suala zima la maendeleo na ndiyo siri ya maendeleo yenu, pia jengeni tabia ya kuwahoji viongozi pale mnapoona wanakwenda kinyume na acheni tabia ya kuwaombaomba fedha,"anasema Bw.Mkina.

No comments:

Post a Comment