11 January 2013
TASO: Katiba ijayo iondoe migogoro ya ardhi nchini
David John na Rehema Maigala
CHAMA cha Wakulima nchini (TASO), jana kiliwasilisha maependekezo yake kwa Tume ya Katiba wakitaka Katiba ijayo iondoe migogoro ya ardhi iliyopo kati ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza Dar es Salaam jana mara baada ya kuwasilisha maoni yao, Mwenyekiti wa chama hicho, Engelebeth Moyo, alisema migogoro ya ardhi kwa makundi hayo inachangia wananchi
kupoteza maisha kwa ajili ya kugombea ardhi.
Bw. Moyo alisema, Serikali imekuwa ikinadi sera mbalimbali za kilimo ikiwemo ile ya Kilimo ni Uti wa Mgongo na Kilimo kwanza, lakini usimamizi wake umekuwa duni kiasi cha wakulima kulalamika siku hadi siku kwa kukosa mahitaji muhimu
ili waweze kuboresha kilimo chao.
“Migogoro mingi ya wakulima na wafugaji inachingiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa mitaa na vijiji, wakati mwingine wamekuwa wakiuza maeneo yanayotumiwa kwa ajili ya
kilimo au mifugo, Katiba ijayo isema wazi kuwa suala la
ardhi liwe chini ya Serikali Kuu au idara maalumu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba la Wafugaji Bw. Daud Haraka, alisema migogoro yote inayojitokeza kati yao na wakulima yanachingiwa na Serikali kutokuwa na sera madhubuti kuhusu mgawanyo wa maeneo.
Sababu nyingine ni kukosekana usimamizi wakutosha kuhusu ardhi hivyo Katiba ijayo itamke wazi kuhusu sera ya ardhi.
“Serikali imewapa kisogo wafugaji ndiyo maana wananyanyasika hata kupata maeneo ya kulishia wanyama ni tatizo, wakati mwingine husababisha migongano kati ya wafugaji na wakulima,” alisema.
Alisema Tanzania ina maeneo mengi lakini Serikali imekuwa ikiyatoa kwa wawekezaji bila utaratibu tena yale yanayotumiwa
na wafugaji pamoja na wakulima.
Bw. Haraka alidai kushangazwa na Serikali kushindwa kumaliza migongano iliyopo kati ya wafugaji na wakulima ambapo wakati mwingine, viongozi wa Serikali za Mitaa, kijiji kushindwa kuwajibishwa kwa kusababisha vurugu hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment