11 January 2013
Hukumu mshtakiwa wa Rais Mwinyi kutolewa Febr. 12
Na Rehema Mohamed
HUKUMU ya mshtakiwa Bw. Abdalah Mzome anayedaiwa kumwibia Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, imepangwa kutolewa Februari 12 mwaka huu.
Pande zote zimemaliza ushahidi wao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambapo mshtakiwa alitoa utetezi wake jana mbele ya Hakimu Gane Dudu, anayesikiliza kesi hiyo.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kumuibia Mzee Mwinyi zaidi ya sh. miloni 37.44 zinazotokana na pango la nyumba.
Awali akitoa utetezi wake, mshtakiwa aliieleza Mahakama hiyo kuwa, Mzee Mwinyi amemfungulia kesi hiyo ili asiweze kutimiza ahadi aliyoitoa kwake ya kumjengea nyumba.
Alidai kuwa, Mzee Mwinyi alitoa ahadi hiyo katika mazungumzo yao ya kawaida baada ya kumfanyia kazi mbalimbali kwa uaminifu mkubwa na hatimaye kumchukulia kama sehemu ya familia yake tangu mwaka 1996.
Aliongeza kuwa, yeye na mlalamikaji kwa muda mrefu walikuwa
na mahusiano mazuri yaliyojenga uaminifu wa kumtuma kaze
zenye fedha nyingi na kumlipa ujira kidogo.
Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na kumtafutia nyumba alizotaka kununua eneo la Mikocheni, Msasani na kumkabidhi fedha za kununulia nyumba hizo zaidi ya sh. milioni 300.
Alidai ununuzi wa nyumba hizo ulikuwa wa siri kati yake na mlalamikaji na baada ya manunuzi kukamilisha, walizifanyia matengenezo na kuweka wapangaji.
“Tumefanya vitu vingi na Mzee Mwinyi kwa siri hata familia yake ilikuwa haiju, nilikuwa na uwezo wa kumuibia fedha za ununuzi wa nyumba alipokuwa ananikabidhi lakini sikufanya hivyo,” alidai.
Hata hivyo, mshtakiwa alikiri kuwa yeye ndiye aliyekuwa akipokea kodi za wapangaji katika nyumba hizo na kumkabidhi Mzee Mwinyi pamoja na mikataba ya wapangaji wanapomaliza kulipa pango na hawakuwa wakisainishana mahali popote kwa sababu waliaminiana.
Huku akitokwa na machozi, mshtakiwa huyo alidai kuwa, mashtaka yanayomkabili ni uonevu na anashangaa kuona Mzee Mwinyi anamtuhumu kumuibia fedha ambazo hakuzichukuwa.
“Kipindi chote nilichokuwa na Mzee Mwinyi, ningeweza kuwa na ghorofa au gari la kifahari kutokana na fedha alizokuwa akinipa nimfanyie kazi zake lakini sikuwa na roho hiyo,” alidai.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, mshtakiwa huyo alidai hataleta mashahidi wengine kwa sababu wengi ni wanafamilia ya Mzee Mwinyi hivyo hawatamtetea ipasavyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment