07 January 2013
Polisi lawamani kwa kupokea rushwa
Na Abdallah AmiriIgunga.
WAKAZI wa Wilaya Igunga, mkoani Tabora, wamesema baadhi
ya askari polisi wilayani humo ni vinara wa kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wananchi.
Tuhuma hizo zimetolewa juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani humo ambapo wananchi hao walidai kuwa, pamoja na Serikali kukemea vitendo hivyo kwa watumishi wa
sekta mbalimbali, Jeshi la Polisi linapaswa kuwafukuza kazi
baadhi ya polisi ambao wanalitia aibu jeshi hilo.
Mkazi wa Wilaya hiyo, Bw. Ayubu Juma, alisema kuwa yeye alikamatwa na askari wa Kitengo cha Usalama Barabarani akiwa
na pikipiki, kupelekwa kituoni na kufunguliwa kesi kwa madai ya
kuendesha chombo hicho bila kuwa na leseni, kofia ngumu.
“Kilichonishangaza, wakati nakamatwa nilikuwa na leseni pamoja na kofia ngumu lakini bado nimefunguliwa kesi ya kubambikiwa kosa, nilipelekwa Mahakamani na kulazimika kukiri mashtaka yote hivyo nilitozwa faini ya sh. 100,000.
“Baada ya kulipa, nilikwenda kituoni kuchukua pikipiki yangu, nilimkuta Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Wilaya ambaye alimwomba shs. 60,000 ndipo nikabidhiwe chombo changu pamoja na kumuonesha stakabadhi ya malipo lakini alikataa,” alisema.
Malalamiko mengine yaliyotolewa katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Elibarik Kingu ni pamoja na kipigo wanachokipata baada ya kukamatwa kwa
makosa mbalimbali na kusababisha wapate ulemavu wa maisha.
“Itakuwa vugumu kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwani mtu anapokamatwa na akabainika ana makosa ni wajibu wa polisi kumfikisha mahakamani badala ya kuanza
kumtesa na kumpiga bila sababu za msingi,” walisema.
Kwa upande wake, Bw. Kingu amepokea malalamiko hayo na kusema hayupo tayari kuona mtumishi yeyote akifanya vitendo hivyo na kusisitiza atalifuatilia suala hilo, kulitolea majibu na kumuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ahakikishe kijana huyo
anapatiwa pikipiki yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment