07 January 2013

Kidoda: CCM haipo vizuri kiuchumi



Na Yusuph Mussa, Handeni

MBUNGE wa Handeni, mkoani Tanga, Dkt. Abdallah Kigoda, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kipo katika hali mbaya kiuchumi mkoani humo, hivyo jitihada binafsi na mikakati madhubuti inahitajika ili kukinusuru.

Dkt. Kigoda aliyasema hayo juzi katika Kikao cha Kamati ya Siasa wilayani humo ambacho mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Dkt. Henry Shekifu.

Katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe watoa kero mbalimbali zinazochangia chama hicho kishindwe kupiga hatua.

“Chama chetu kipo nyuma kiuchumi katika Mkoa huu, tuweke mkakati maalumu wa kukuza uchumi pamoja na kuznisha miradi
ya maendeleo,” alisema Dkt. Kigoda ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara.

Diwani wa Kata ya Kideleko, Bw. Mohamed Mwatangulu, alisema kadi za CCM zimekuwa adimu kupatikana kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo aliomba zipelekwe kwa wingi ili wananchi hasa vijana waweze kuzipata.

“Wenzetu vyama vya upinzani wanagawa kadi kama njugu, wakati mwingine wanazigawa bure hata kwa watu wasio na mwelekeo lakini sisi kupata kadi za CCM ni ngumu...kuwe na utaratibu wa kuzipata mara kwa mara” alisema Bw. Mwatangulu.

Akijibu hoja za wajumbe, Dkt. Shekifu alisema CCM mkoani humo si kwamba haina miradi bali udhibiti wa mapato na matumizi haupo katika miradi hiyo hivyo ataunda Kamati ya Udhibiti wa Mapato na Matumizi ambayo itasimamia miradi yote ukiwemo Uwanja wa Mkwakwani na maduka yanayozunguka uwanja huo.

Alisema ni muhimu kutolewa kwa kadi za CCM lakini kwa tahadhari kubwa ili zisije kuchukuliwa na mamluki ambao watakifanya chama hicho kishindwe kushika dola 2015.

“Japo kupata wanachama ni muhimu, kuwahakiki ni muhimu zaidi, tuwe waangalifu msije mkaingiza wanachama mamluki wakaja kutupa shida katika Uchaguzi Mkuu 2015,” alisema.

Aliwataka wana CCM wawe macho hasa na watendaji wa halmashauri ambao baadhi yao wanatengeneza kero za wananchi wanazitengeneza ambazo wakati mwingine si kubwa na zinaweza kupatiwa ufumbuzi lakini wanakuwa hawajali.

Dkt. Shekifu alihadharisha suala la ardhi na kudai linaweza kukifanya chama hicho kisiendelee kushika dola mwaka 2015
kama watashindwa kulipatia ufumbuzi ambapo matatizo ya wananchi kuhusu ardhi ni mengi na linachangiwa na
wahamiaji kutoka mikoa ya Manyara na Arusha.

“Mkiwa legelege mtashindwa kuisimamia Serikali, kero nyingi zinaibuliwa na Watendaji wa halmashauri ambao wanachangia kukihujumu chama chatu.

“Kwa mfano, matatizo ya maji si makubwa kiasi cha kushindwa kupatiwa ufumbuzi lakini kero ya ardhi kwa wananchi ni tishio kwa CCM mwaka 2015,” alisema Dkt. Shekifu.

No comments:

Post a Comment