Anneth Kagenda na Rehema Maigala
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam Ramadhani Madabida, amewajia juu baadhi ya viongozi wa CCM kwa kumtuhumu kutoa nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa madai ya kulipa fadhila baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti.
Kauli ya Mwenyekiti huyo imekuja baada ya gazeti moja la kila siku (sio Majira) lililolipoti kuwa Madabida anawapa uongozi baadhi ya watu kwa nia ya kulipa fadhila za kumchagua kutokana na malalamiko ya baadhi ya wanachama ndani ya mkoa huo.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, alisema wanachama wanaosema hayo wamemvunjia heshima pasipo kujua kwamba yeye alichaguliwa kwa kura 310 kutokana na mambo mazuri aliyoyafanya na yale anayoendelea kuyafanya.
"Ni ukweli usiopingika kwamba hawa wamenivunjia heshima na kuonekana kwamba nilipachikwa uongozi wakati nilishinda kwa kura nyingi kutokana na kwamba walionichagua wananikubali na wanajua mambo mazuri ninayoyafanya ndani ya chama," alisema.
Aliongeza kuwa kiongozi au mwanachama anayejadili mambo ya vikao vya chama kwenye vyombo ya habari ni kukiuka taratibu na kanuni za chama zilizopo.
"Kwa nini mtu anabeba maneno yanayofanyika ndani ya chama na kuyapeleka kwenye vyombo vya habari...ninachojua mimi mambo ya chama yanamalizwa kwenye vikao vya chama na si vinginevyo na kama kuna malalamiko zipo taratibu zetu ndani ya chama na wao wanazijua,"
Akizungumzia kuhusu uchaguzi, alisema kwenye uchaguzi wowote wapo wanaoshinda na wanaoshindwa na kwamba wapo wanaotaka uongozi kwa kutumia fedha hivyo mambo kama hayo lazima yajitokeze katika chaguzi zote.
Madabida, alikanusha kuwa CCM haina kamati ya wajumbe wa ulinzi na usalama badala yake kamati hizo ziko kwenye vyombo vya dola na kutolea mfano kuwa ziko kwa wakuu wa wilaya ambao mwenyewe ndiye anakuwa mwenyekiti
Hata hivyo alisema ataendelea kusimamia na kutenda haki kutokana na kwamba sifa hiyo anayo na kwamba hata siku moja hakuna mwanachama ambaye aliwahi kumfata kwa tatizo la kichama akashindwa kumsaidia, kumwelekeza au kumwambia kuwa analolizungumza anahaki au la.
"Mwanachama akija kwangu anauhakika wa kupata ufumbuzi wa kile alichojia na hiyo ndiyo kawaida yangu hivyo basi ninawaasa hawa wanaoenda kwenye vyombo vya habari waache mambo hayo yamalizwe ndani ya chama na si vinginevyo kwani masuala yetu yanamalizwa na vikao na si kupitia kwenye vyombo hivyo," alisema Mwenyekiti Madabida.
No comments:
Post a Comment