07 January 2013

Lieweg:Kila kitu kitakaa sawa Oman



Speciroza Joseph, Zanzibar

WIKI chache kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, Kocha wa Simba, Patrick Liewig amesema programu ya maandalizi itamalizika nchini Oman tayari kwa kuanza ligi.

Akizungumza visiwani hapa, kocha huyo alisema kushiriki Kombe la Mapinduzi ni moja ya sehemu ya maandalizi kwa ajili ya ligi kuu na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Alisema baada ya kumaliza mashindano hayo timu kamili itakwenda nchini Oman kwa ajili ya mazoezi ya mwisho na itakaporejea ligi itakuwa inakaria kuanza.

"Tukimaliza mashindano haya, tutakuwa tupo vizuri, kwa pamoja tutakwenda  Oman kukamilisha programu ya mazoezi na maandalizi kwa ajili ya ligi kuu" alisema kocha Liewig.

Akiongeza kuwa katika siku chache tangu aliojiunga na timu hiyo imeonyesha kubadilika na kuwa vizuri tofauti na alivyoikuta, hivyo wakikamilisha maandalizi hayo itakuwa tayari kupambana na kutetea ubingwa wake.

Kocha huyo alisema wachezaji wote wakishajiunga na timu hiyo na kuanza mazoezi ya pamoja atapata nafasi nzuri ya kujua uwezo na viwango vya kila mchezaji ili kuwatengeneza vizuri.

Simba inashiriki kombe hilo, imeshacheza mechi mbili  kabla ya jana usiku, imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Jamhuri 4-2, ikatoka sare ya 1-1 na timu ya Tusker ya Kenya.

Kocha huyo katika michezo yote amekaa jukwaani na kutoa maelekezo kabla ya kuanza mechi na kipindi cha mapumziko kwa makocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' na Moses Basena wanaokaa kwenye benchi la ufundi kuisimamia timu hiyo.

No comments:

Post a Comment