11 January 2013

Kisandu apewa cheo NCCR



Na Benedict Kaguo

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimemteua Bw. Deogratius Kisandu kuwa Katibu wa Mahusino na Uenezi Kitengo cha Vijana baada ya kujiunga na chama hicho hivi karibuni.


Bw. Kisandu ametokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambako alikuwa Katibu wa Baraza la Vijana
(BAVICHA), mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa barua ya uteuzi iliyoandikwa na Ofisa Tawala
wa NCCR-Mageuzi, Bw. Florian Rutayuga ambayo gazeti hili
inayo nakala yake, alisema uteuzi huo umeanza Januari 8,2013.

“Napenda kukuarifu kwamba, kuanzia kuanzia tarehe ya barua hii,
nimekuteua kuwa Katibu wa Mahusino na Uenezi Kitengo cha Vijana wa NCCR-Mageuzi.

“Uteuzi huu ni kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 39(g), ya toleo la pili lililohaririwa mwaka 2003 la kanuni za kitengo cha vijana NCCR-Mageuzi mwaka 2000,”
ilisema barua hiyo.

Akizungumzia uteuzi huo, Bw. Kisandu alisema nafasi aliyopewa ameipokea kwa furaha kubwa kutokana na chama hicho kutambua uwezo wake kisiasa na Mwenyekiti wa chama hicho Taiga, Bw. James Mbatia, kumpa moyo wa kuitumikia.

“Jukumu nililopewa ni pamoja na kuandaa kauli mbiu inayosema 'Vijana ni Rasilimali ya Taifa', lengo ni kuhakikisha kuanzia sasa, milango iko wazi ili waweze kulitumika Taifa.

“Kazi ya ukombozi wa pili wa Taifa hili iko mikononi mwao na wasikubali kufanya maandamano yenye faida kwa viongozi
badala ya wananchi,” alisema Bw. Kisandu.

Aliyataja majukumu aliyopewa kuwa ni pamoja na kuandaa wagombea ubunge na udiwani 2015 kupitia idara ya vijana nchi nzima, kusimika viongozi katika majimbo yote nchini na kuandaa kikosi kazi cha ushindi kwa vijana kila Wilaya ili kuhakikisha
vijana wanashika hatamu ya uongozi nchi nzima.

1 comment:

  1. Vijana kuweni na msimamo kama mna nia ya dhati ya kuikomboa TZ. Suala la kuhama CDM na kuhamia NCCR halafu kupewa wadhifa on the spot kidogo inaleta wasiwasi. Huenda ndugu huyu alirubuniwa ili ahame chama chake cha awali kwa kupewa ahadi ya kupatiwa cheo. Hata huko NCCR huenda akahama akaenda chama kingine ambacho kitakuwa tayari kumtunuku cheo zaidi. Hizo ni tamaa za kidunia.

    ReplyDelete