08 January 2013

JUKUILA yagawa viwanja kwa wanachama 100


Na Heri Shaaban

JUMUIYA ya Kukuza Uchumi, Wilaya Ilala Dar es Salaam (JUKUILA), imegawa viwanja vilivyopo eneo la Zingiziwa,
Kata ya Chanika, kwa wanachama 100 ambao wamejiunga
na jumuiya hiyo.

Ugawaji wa viwanja hivyo ulifanyika Dar es Salaam jana, ambapo Mwenyekiti wa JUKUILA, Bw. Mussa Salum, alisema viwanja hivyo vimetolewa kwa kila mwanachama aliyetimiza masharti.

Alisema lengo la jumuiya hiyo ni kuhakikisha wanachama wake wanapata maeneo ya kujenga nyumba ili kujiletea maendeleo.

“Wanachama 100 waliojiunga na jumuiya hii, tumewagawia viwanja vyenye ukubwa wa mita 25 kwa 16 sawa na ukubwa wa robo heka ili waweze kujenga nyumba za kuishi au kuweka miradi ya maendeleo,” alisema Bw. Salum.

Aliongeza kuwa, jumiya hiyo ilianzishwa mwaka 2010 ikiwa
na wanachama 1,800 na vikundi zaidi ya 600 vya kukopeshana ambapo eneo la Zingiziwa wamewekeza shamba lenye ukubwa
wa heka 130.

“Kila mwanachama ambaye amejiunga kwenye kikundi analipia sh. 700,000 ndipo aweze kupewa kiwanja, Serikali ya Mtaa Zingiziwa inamkabidhi hati ya muda kama mkazi wa eneo husika wakati tukisubiria taratibu za manispaa za kupata hati miliki.

“Eneo hili bado halijapimwa na Manispaa ya Ilala, changamoto zilizopo ni vikundi vilivyopo katika jumuiya havirejeshi fedha za mikopo kwa wakati unaotakiwa,” alisema.

Aliziomba taasisi mbalimbali za kifedha nchini kuisaidia jumiya hiyo iweze kupata mikopo ya riba nafuu ili kuwainuwa wanachama wake kwa kuwakopesha vifaa vya ujenzi waweze kujenga nyumba katika maeneo waliyopewa.

No comments:

Post a Comment