02 October 2012

TIPF wamtaka Slaa aache kumuandama Lowassa


Na Anneth Kagenda

MKURUGENZI wa Taasisi ya Islamic Peace Foundation (TIPF), Bw. Sadiki Godigodi, amemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, kuacha kumuandama Waziri Mkuu aliyejiuzulu Bw. Edward Lowassa na Mbunge wa Bariandi Magharibi Bw. Andrew Chenge.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Godigodi, alisema uamuzi uliofanywa na Kamati Kuu (CC), kuwaacha wanachama hao wagombee nafasi walizoomba ulikuwa sahihi hivyo Dkt. Slaa hakupaswa kuupinga.

Alisema kupitishwa kwa majina ya Bw. Lowassa na Bw. Chenge kutakiimarisha chama hicho, kujenga umoja na mshikamano kwani kama majina yao yasingerudi, kungetokea mpasuko mkubwa.

Aliwataka wana CCM kumpa ushirikiano Bw. Lowassa kwani dalili zinaonesha kuwa wapinzani wanamuogopa.

“Watanzania wanaelewa jinsi alivyokuwa mchapa kazi hodari, amejituma sana pia ni mtu anayejitoa kwa watu na kuwapa misaada ya hali na mali,” alisema.

Bw. Godigodi aliongeza kuwa, Bw. Lowasa ni mfano wa kuigwa na anastahili pongezi kwa jinsi anavyojitoa kuisaidia jamii ya kada mbalimbali, taasisi za dini na binafsi.

“Hivi karibuni alikabidhi msaada wa madawati 500 katika Shule ya Msingi Kipawa, hoja ya ufisadi inayotolewa na Dkt. Slaa hazina mashiko kwani suala la rada lilishatolewa maelezo na Serikali ya Uingereza sasa kama yeye anao ushahidi, kwanini asimpeleke mahakamani,” alihoji Bw. Godigodi.

Alisema wao kama taasisi na sehemu ya jamii ya Watanzania wanapongeza uamuzi mzuri uliofanywa na CCM kupitisha majina yao ili waweze kuwania uongozi na kumpinga Dkt. Slaa.

4 comments:

  1. Hata angesafishwa kwa kiasi gani ni fisadi tu.
    Wanaomwogopa ni CCM wenyewe si watu wengine.Waislamu malizeni matatizo yenu kwanza siasa hamziwezi.

    ReplyDelete
  2. GODIGODI KASHAPEWA PESA ZA KIFISADI.

    ReplyDelete
  3. Ama kweli pesa sabuni ya roho na penye udhia penyeza rupia! Taasisi ya kiislamu? Kuwatetea Lowassa na Chenge? Binafsi siamini kwamba hiyo taasisi inawakilisha uislamu au waislamu kwani yaliyotendwa na mabwana hawa yanastahili kukemewa na dini ya imani yoyote inayomkiri Mungu isipokuwa ile ya kusali usiku, waumini wao wakiwa watupu ambayo mungu wao tunamjua.
    Namwomba Bwana Godigodi akome kuudhalilisha uislamu kwa njaa yake ya siku moja.

    ReplyDelete