01 August 2012

Yanga SC yamkuna Azima Dewji



Na Mwandishi Wetu

MWANACHAMA maarufu wa Klabu ya Simba, Azim Dewji ameipongeza timu ya soka ya Yanga kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame.

Yanga ilinyakua ubingwa huo mwishoni mwa wiki, baada ya kuizamisha Azam kwa mabao 2-0 katika mchezo wa fainali iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Dewji ambaye aliwahi kuifadhili Simba na kuifikisha
katika fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, alisema pamoja na yeye kuwa Simba 'damu’, ana kila sababu za kuimwagia sifa Yanga kwa kuwa imezika haraka
matatizo yake na kugeukia kusaka maendeleo.

“Huwezi kuamini kama Yanga iliyopigwa mabao 5-0 na kuibua tafrani nzito Jangwani, ndiyo hii ya leo. Wameikubali hali na kubadilika ndani ya
muda mfupi mno.

"Wana amani na matunda yake yameonekana ingawa
walikuwa na kipindi kifupi cha kusuka timu na kurejesha mshikamano ndani ya klabu.

“Naipongeza Yanga na hasa Mwenyekiti wake, Yussuf Manji kwa sababu naamini imani ya wanachama juu yake ndiyo iliyorekebisha hali haraka, naye kama kiongozi kuhakikisha usajili makini unafanyika, kocha
anapatikana na uzalendo ndani ya Yanga unarejea,” alisema Dewji.

Aliongeza kuwa, pamoja na matunda ya haraka ya uongozi wa Manji, wana-Yanga wanapaswa kumpa ushirikiano ili kuiondoa Yanga katika
utegemezi wa miaka nenda rudi, huku akisisitiza Manji hatabaki Yanga milele.

“Wana kiongozi shupavu, sasa washirikiane naye kuujenga uchumi wa klabu. Haya mambo ya kutegemea mtu kila kukicha si mazuri. Na hili si kwa Yanga tu, hata Simba na klabu nyingine zinapaswa kujikita katika
kujijenga kiuchumi ili ziwe na jeuri ya fedha bila ya kutegemea mifuko ya mwanachama mmoja mmoja,” alisema.

Akisisitiza kujijenga kiuchumi, Dewji mmoja wa wafanyabiashara maarufu nchini alisema viongozi wa Klabu kubwa za Simba na Yanga zianze kuutumia mtaji wa wanachama kujijenga, huku akitolea mfano kuwa, kila moja ina zaidi ya wafuasi milioni 15, lakini klabu zinabaki kuwa masikini.

“Huu ni mtaji mkubwa mno, lakini utashangaa klabu haina hata asilimia moja (150,000) ya wanachama wa kweli. Kila siku utasikia wanachama
3,000 hadi 6,000. Kiongozi wa klabu anachaguliwa na wanachama wasiofika 2,000?

“Jamani, kwa klabu inayoshabikiwa na mamilioni ya watu inashindwaje kujijenga kiuchumi kwa kuwatumia mashabiki wake waliozagaa kila kona ya nchi? Jiulize, kama angalau hao watu 150,000 tu wakilipa ada ya
mwaka ya 12,000 ambayo hata hivyo bado ni ndogo, si wanaweza kuvuna sh. bilioni 1.8 kwa mwaka, hizi si fedha nyingi?

“Kuna haja ya kufanya mapinduzi ya kweli, badala ya kufikiria kuifunga Simba au Yanga na kutwaa ubingwa wa Bara. Timu yenye uchumi imara, ndiyo inayokuwa na jeuri ya kuwa na kikosi imara na hivyo kufanya
vizuri zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Huko ndiko tunakopaswa kwenda,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment