01 August 2012

WALIMU NCHI NZIMA HAWASHIKIKI

Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani

MGOMO wa walimu ulioanza juzi katika mikoa mbalimbali nchini, jana umezidi kushika kasi mkoani Morogoro ambapo katika Shule ya Msingi Mkekena, Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya wazazi shuleni hapo Bw. Ibrahim Piia, aliwataka walimu walioshiriki mgomo wasirudi tena hata kama Serikali itawalipa madai yao.


Bw. Piia alitoa kauli hiyo baada ya kufika shuleni hapo kuangalia athari za mgomo ambapo wanafunzi wa shule hiyo walilazimika kurudi nyumbani baada ya Mwalimu Mkuu, Bw. Rueben Mbaga, kuwaruhusu kwa sababu hakukuwa na walimu wa kuwafundisha.

Alisema wazazi wa wanafunzi, wameilalamikia kamati ya shule hiyo wakitaka walimu waliogoma kuanzia juzi huku wakijua wanafunzi wa darasa la saba wapo mbioni kufanya mitihani wasirudi shuleni hata kama mgomo huo utapatiwa ufumbuzi.

“Naunga mkono kauli ya wazazi waliolalamika kwani kitendo cha wanafunzi kurudishwa nyumbani wakati waanakabiliwa na mitihani ni unyama unaolenga kuwafelisha,” alisema.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Shule ya Msingi Kulangwa, iliyopo Kata ya Goba, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, juzi imewarudisha wanafunzi nyumbani kutokana na mgomo huo.

“Walimu wenzetu nchi nzima wamegoma hivyo tunawaunga mkono, hakuna mwalimu ambaye ataingia darasani kufundisha hadi madai yetu yapatiwe ufumbuzi,” ulisema uongozi huo.

Iramba mkoani Singida

Katika Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, mgomo huo jana uliendelea kwa siku ya pili ambapo zaidi ya walimu 1,762 wamegoma ili kuishinikiza Serikali iwalipe madai yao.

Hata hivyo baadhi ya walimu walienda kazini kusaini vitabu vya mahudhurio na kurudi nyumbani na wengine kubaki maeneo ya shule wakirandaranda.

Katibu wa CWT wilayani hapa, Bw. Jumbe Semgunda, akiwa Mwenyekiti wake, Bw. Hamisi Kumala, walisema mgomo huo ni halali kwani umezingatia taratibu zote.

Wilaya ya Korogwe

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, jana alimuagiza Mkuu wa Polisi wilayani hapo (OCD), amkamate Katibu wa Chama cha Walimu nchini (CWT), Wilaya ya Korogwe Bw. Festo Mitimingi kwa kuhamasisha mgomo wa walimu.

Alisema walimu wote wanaogoma, atawatoa kwenye orodha ya kuandikisha Sensa ya Watu na Makazi Agosti 26 mwaka huu pamoja na kuingia kwenye Shule za msingi Mjini Korogwe na kufundisha baadhi ya masomo.

Kwa upande wake, Bw. Mitimingi alisema haogopi kuwekwa ndani kwa huo ni mgomo halali na unafanyika nchi nzima na kudai kuwa, Bw. Gambo amekiuka sheria ya kitaaluma kwa kuingia madarasani na kufundisha wanafunzi.
CWT Mkoa wa Dar es Salaam

Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Dar es Salaam, kimewataka walimu kuendelea kushikamana katika kipindi hiki cha mgomo ili kuhakikisha wanapata stahiki zao bila kuogopa vitisho.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Bi. Zubeda Aziz, alisema zipo taarifa za vitisho mbalimbali zinazotolewa kwa walimu waliogoma.

“Serikali inaendelea kutoa vitisho ili walimu waogope lakini ielewe kuwa, kama wataendelea navyo badala ya walimu kukaa nyumbani tutaanzisha mgomo baridi wa kwenda kazini lakini hatufunidhi.

“Mwenye mamlaka ya kufukuza mwalimu kazini ni Bodi ya Tume ya Utumishi wa Walimu ya Wilaya (TSD) iliyoundwa na watu ambao si viongozi wa Serikali, hivyo walimu endeleeni kukaa nyumbani hadi Rais CWT, Bw. Gratian Mkoba atakapotoa mwongozo,” alisema.

Aliongeza kuwa, Serikali bado ina nafasi ya kukaa chini na walimu ili kupata ufumbuzi ambapo katika Mkoa huo, zaidi ya walimu 11, 500 kati 12, 4047 waliunga mkono mgomo huo.

Musoma mkoani Mara

Hali ya mgomo katika mji wa Musoma, mkoani Mara, jana  imechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kuwatia mbaroni baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Molembei waliokuwa wakiandamana kudai haki ya kufundishwa.

Wanafunzi waliokamatwa ni saba na walifanya maandamano baada ya walimu wao kutoonekana katika maeneo ya shule hivyo kubaki wakiwa hawana mwalimu wa kuwafundisha.

Wilaya ya Bunga

Mgomo huo katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, jana uliendelea kwa mtindo wa aina yake baada ya wakuu wa shule waliamua kuwafungia wanafunzi zaidi ya saa nne ndani ya vyumba vya darasa.

Baadhi ya viongozi wa CWT wilayani humo walionekana wakizunguka katika baadhi ya shule na kushinikiza walimu wasiogoma waunge mkono mgomo huo.

Wanafunzi waliofungiwa hawakupata nafasi ya kwenda mapumziko hadi walipofunguliwa saa saba mchana na baadaye kuruhusiwa kwenda nyumbani ambapo baadhi ya wazazi walionesha kukasirishwa na kitendo hicho.

Mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya walimu wakifika shuleni, kusaini daftari la mahudhurio na kurudi nyumbani huku wanafunzi wakirudishwa wakibaki bila walimu. Miongoni mwa shule ambazo wanafunzi walirudishwa ni Shule ya Msingi Kabarimu.

Wilaya ya Moshi, Kilimanjaro

Walimu katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, jana walikusanyika vikundi katika maeneo yao ya kazi badala ya kuingia darasani ili kufundisha wanafunzi.


Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi mkoani hapa limewahadharisha walimu kutowatumia wanafunzi kudai haki zao, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na haki za watoto.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, alisema hakuna haja ya watoto kuingizwa katika malumbano na maandamano yasiyo na tija na walimu ambao watabainika kuwashawishi watachukuliwa hatua za kisheria.

Hali ya mgomo Dar

Hali ya mgomo katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam, imezidi kuwa mbaya ambapo katika baadhi ya shule, watu wasio na taaluma hiyo waliingia madarasani kufundisha wanafunzi.

Akizungunza na gazeti hili, Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mwananyamala Kisiwani, Bw. Method Rugambalala, alisema shule hiyo ina wanafunzi 1,500 na walimu 32.

Alisema kutokana mgomo, baadhi ya watu wasio na taaluma hiyo wamejitokeza na kuingia madarasani kufundisha wanafunzi wa darasa la nne hadi sita na wanafunzi wa darasa la saba walikuwa wakifundisha  na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Bw. Ramadhani Lulela, ambaye kitaaluma ni Mhasibu.

Katika hatua nyingine, wanafunzi katika Shule ya Msingi Kinondoni, walisema jana walifika shuleni mapema lakini ilipotimu saa nne asubuhi, waliruhusiwa kurudi nyumbani.

Katika Shule ya Msingi Makamba iliyopo Tandika, wilayani Temeke, idadi kubwa ya walimu hawakufika shuleni wengine wakisaini vitabu vya mahudhurio na kuondoka.

Hali hiyo ilisababisha mahudhurio ya wanafunzi kupungua kutoka asilimia 63 hadi 47 na ifikapo mchana hali ikawa mbaya zaidi.

Shule ya Msingi Bologani, iliyopo Mtoni Mtongani kulikuwa na  walimu 26 kati ya 48 hivyo wanafunzi kurudishwa nyumbani ambapo katika Shule ya Msingi Tandika Mabatini, wanafunzi walikuwa wakipewa jukumu la kufanya usafi.

Katika Shule ya Msingi Makamba, iliyopo Tandika, idadi kubwa ya walimu hawakufika shuleni wengine wakisaini vitabu vya mahudhurio na kuondoka hivyo kusababisha mahudhurio ya wanafunzi kupungua kutoka asilimia 63 hadi 47.

Kamanda Kova azungumza

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Suleiman Kova, jana alijitosa katika sakata hilo na kuahidi kufanya uchunguzi dhidi ya kundi linalodaiwa kuwafanyia fujo walimu ambao hawajagoma.

“Natoa mwito kwa walimu na wanafunzi watakao bughudhiwa au kutishiwa, watoe taarifa mara moja,” alisema Kamanda Kova.

Mkoani Arusha

Katika Mkoa wa Arusha, zaidi ya walimu 1,000 wa shule za msingi ndani ya Manispaa ya Arusha, wameungana na wenzao waliogoma kwa ili kushinikiza kutekelezwa kwa madai yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Elimu Manispaa ya Arusha, Bw. Omary Mkombole,  alisema mgomo huo umeanza juzi lakini walimu wamegawanyika katika makundi matatu.

Alisema wapo walimu wanaokwenda shuleni bila kufundisha, wanaofika na kusaini na kundi la mwisho hawafiki kabisa.

Jiji la Mbeya

Katika Jiji la Mbeya, mgomo huo umechukua sura mpya baada ya walimu wengi kutofika shuleni kabisa tofauti na juzi.

Akizungumza na gazeti hili, Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya
Msingi Gombe, iliyopo Uyole, Bi. Getruda Konga, alisema siku ya jana hakuna mwalimu aliyefika shuleni.

Shule ya Msingi Mwasote ya Uyole, hali haikuwa shwari ambapo walimu 10 kati ya 22, ndio waliofika kazini, kusaini kitabu cha mahudhuria na kurudi nyumbani.

Kamanda wa Polisi wa mkoani hapa, Diwani Athmani, alisema baadhi ya walimu wanashikiliwa kwa kuhamasisha mgomo.

Aliwataja walimu hao kuwa ni Patro Mangula (52),  Emmanuel Kyejo (45), Anyakingwe Lwingwa (45) na Akson Kibona (52).

Wilayani Muleba

Walimu katika Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, wameendelea kuungana mkono mgomo huo ili kuishinikiza Serikali ifanyie kazi madai yao.

Baadhi ya shule za msingi na sekondari zilizotembelea na gazeti hili kulikuwa hazina walimu huku wanafunzi wakiendelea kucheza na wengine wazurura mitaani.

Ofisa Elimu Shule za Sekondari wilayani Muleba. Bw. Julius
Kakyama, alikiri mgomo huo kuendelea licha ya tamko la Serikali kuwataka warejee kazini wakati madai yao yakiendelea kutafutiwa ufumbuzi.

Alisema takwimu za jana zinaonesha kuwa, walimu 129 wa shule za sekondari walikuwa wamegoma na wengine 165 wakiendelea na kazi ambapo walimu wa shule saba za Serikali walikuwa wamegoma na shule 18 walikuwa kazini.

Mkoani Mwanza

Katika Mkoa wa Mzwanza, walimu waliendelea na mgomo ukihusisha wale wa shule za msingi na sekondari isipokuwa zile binafsi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa. walimu wengi walifika kazini, kusaini vitabu vya mahudhurio na kutoingia madarasani kufundisha.

Mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya walimu wakiwa wamekaa
ofisini wengine wakiwa nje ya ofisi wakipiga soga.

Katibu CWT mkoani hapa, Bw. Isaack Shaushi, alisema kwa mujibu wa tangazo hilo, suala la walimu kutokwenda kazini ni utashi wa mtu lakini wao wanataka wasiende kabisa.

Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi

Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, jana  imepanga kutoa uamuzi wake kesho kuhusu ombi dogo ambalo liliwasilishwa na Serikali kuomba zuio la muda la mgomo ili kutoa fursa la kuendelea kusikilizwa kesi ya msingi iliyopo mahakamani hapo.

Jaji anayesikiliza shauri hilo, Sofia Wambura, alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za pande mbili kati ya Serikali na CWT.

Wakili wa Serikali Mkuu, Bw. Obadia Kamea, aliiomba mahakama kusitisha mgomo wa walimu akidai ni batili na haujakidhi matakwa ya kisheria ya sheria namba 26 (1) ya utatuzi wa migogoro ya watumishi wa umma.

Alidai CWT walitakiwa watumie sheria hiyo, ambayo inataka upigaji kura ufanyike ndani ya siku 60 badala ya kutumia sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini ambayo inaruhusu mgomo kufanyika baada ya notisi ya saa 48.

“Julai 27, mwaka huu tulikuwa wote hapa mahakamani lakini hawakutupa notisi badala yake, jioni wakatuletea natosi ya saa 48 wakati kwa mujibu wa taratibu za kazi, siku za mapumziko ya mwisho wa wiki hazihesabiki,” alisema.

Akijibu hoja za Serikali, wakili wa CWT, Bw. Gabriel Mnyele, alidai mgomo huo ni halali kwani umefuata sheria husika.

Alidai huo ni muda muafaka wa Serikali kukutana na wafanyakazi wake kufikia makubaliano badala ya kukimbilia mahakamani kuomba zuio la mgomo.

Waandishi wa habari hii ni Bryceson Mathias, Rehema Maigala, Phiesthow Sanga, Yusuph Mussa, Darlin Said,  Gift Mongi, Raphael Okello, Veronica Modesti, Jane Hamalosi, Mariam Said, Anneth Kagenda, Faida Myomba, Neema Malley, Mohamed Mohamed, Queen Lema, Daud Magesa, Livinus Feruzi, Esther Macha, Rehema Mohamed na David John.

2 comments:

  1. WAALIMU WANGU,
    NCHI YETU NI YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA,TUNAISHI KAMA NGUGU, NA TUKUMBUKE AHADI ZA MWANATANU AMBAYO MOJAWAPO ILIKUWA NI "KUJIELIMISHA KWA KADIRIRI YA UWEZO WANU NA KUTUMIA ELIMU YENU KWA FAIDA YA WOTE!PIA MKUMBUKE ELIMU NI WITO!NA ZAIDI UALIMU HAIBA, NISINGEPENDA KUWAPA SHULE WALIMU MLIONIPA UWAZIRI.WALIMU HUWA HATUGOMI TUNALALAMIKA SASA KATIKA MGOMO HUU NINAHISI MAADILI YA UALIMU YAMESHUKA ITABIDI MUENDE JKT KUPATA NIDHAMU.NA HII NI KWA FAIDA YA WALALAHOI AMBAO WATOTO WAO WANASOMA ST KAYUMBA KWANI WATOTO WETU WANASOMA UGHAIBUNI. KAYUMBA.LAKINI MMESIKIA MKWARA HUO WA KUWAFUTA KWENYE ORODHA YA WATAKAOENDESHA SENSA? CHONDE CHONDE WAALIMU HAIBA

    ReplyDelete
    Replies
    1. NDUGU YANGU AHADI ZA MWANATANU NI ENZI YA NYERERE, LEO NYERERE HAYUPO, NCHI IKO MIKONONI MWA MAFISADI AMBAO SIKU ZOTE HUWADHULUMU WALIMU. HAKUNA CHA CHONDE CHONDE HAPA.

      Delete