02 August 2012

Wachezaji Azam 'wamlilia' Stewart


Na Speciroza Joseph

BAADA ya Azam FC kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha wao, Muingereza Hall Stewart, wachezaji wamesikitishwa na kitendo hicho huku kocha huyo akisema ni sehemu ya makubaliano yao kwa maslahi ya klabu na yeye mwenyewe.


Juzi usiku Azam FC walikaa pamoja na kocha huyo na kufikia muafaka wa kusitisha mkataba wake kutokana na mabadiliko katika sera ya klabu hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana na gazeti hili, wachezaji hao (majina tunayo) wameoneshwa kusikitishwa na kitendo cha kocha huyo kuondoka na kusema ameondoka kipindi ambacho wanamuhitaji na hawajapewa sababu ya msingi  kuondoka kwake.

"Ni pigo kwetu kama wachezaji tuliozoea kuwa naye, nimeshangazwa kupata taarifa hizo, sijajua sababu maalum ya kusitisha mkataba, tunasikitika lakini hatuna jinsi," alisema mchezaji huyo.

"Kiukweli tutaathirika kisaikolojia nakumbuka aliondoka kocha wa kwanza kwa sababu kama hiyo na kocha huyo naye hivyo hivyo," alisema mchezaji mwingine ambaye kwa sasa ni tegemezi katika timu hiyo.

Pia walizungumzia madai ya kuwepo kwa mgomo katika timu yao walisema suala hilo halipo kwa kuwa timu inafanya mazoezi kama kawaida na wachezaji wote wanahudhuria.

Naye Stewart akizungumza kwa simu na gazeti hili jana kuhusu kutimuliwa kwake, alisema timu imedhamiria kubadili sera yake kwa kutumia zaidi kukuza wachezaji vijana pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji.

"Tumefikia makubaliano hayo pamoja na Mwenyekiti Abubakar Bakhresa, upande wangu sijaathirika na kitu kwa kuwa vitu vyote vipo sawa na huo ni mtazamo wa klabu," alisema Stewart.

Aliongeza kuwa sababu inayosemwa ya kupoteza mchezo wa fainali sio ya kweli, yalikuwa ni matokeo na mafanikio kwa klabu halikuwa jambo baya kwa kuwa walicheza kwa mara ya kwanza na kuingia fainali.

Aidha kocha huyo aliitakia Azam FC mafanikio mema katika maandalizi yake ya Ligi Kuu na mashindano yajayo na kusema timu kwa kipindi hiki itakuwa chini ya kocha wa vijana Nagul Vivek na kocha msaidizi Kali Ongala.

No comments:

Post a Comment