02 August 2012
Chuji, Redondo, Bahanuzi waitwa Stars
Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Kim Poulsen, amewaita katika kikosi chake viungo Athuman Idd 'Chuji, Ramadhan Chombo 'Redondo na mshambuliaji Said Bahanuzi.
Kocha huyo amewaita wachezaji 21 kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa inayotarajiwa kuchezwa Agosti 15, mwaka huu katika nchi ambayo itatangazwa baadaye.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kim alisema amewaita wachezaji hao baada ya kuridhishwa na uwezo wao, pia wachezaji hao wapya aliowaongeza aliwaangalia katika michuano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.
"Nimeangalia vigezo vinavyotakiwa na pia wachezaji ambao nimewaongeza nimeridhishwa na viwango vyao walivyoonesha katika michuano ya Kagame.
Alisema wachezaji wote wanatakiwa kuripoti kambini kwenye hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Agosti 8 mwaka huu kuanzia saa 1 jioni tayari kwa mazoezi yatakayoanza siku inayofuata.
Alitaja kikosi hicho kwa makipa walioitwa hicho ni Deogratias Munishi (Azam), nahodha Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni nahodha msaidizi Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Moshi (Simba), Mrisho Ngassa (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Ramadhan Chombo (Azam), Ramadhan Singano (Simba), Salum Abubakar (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Wachezaji wanaounda safu ya ushambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samatta (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Said Bahanuzi (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Alisema amewaacha katika kikosi chake kiungo Nurdin Bakari na beki Amir Maftah kwa kuwa ni majeruhi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment