26 July 2012

Serikali yashirikisha asasi binafsi kuboresha huduma



Darlin Said na Angelina Mganga

SERIKALI imeanza mchakato wa kushirikisha asasi zisizo za kiserikali kuboresha huduma kwa umma na kusaidia kuelimisha wananchi ili wadai haki zao na huduma bora.

Naibu Katibu Mkuu Utumishi, Bw. Hab Mkwizu, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano ulioshirikisha Serikali na asasi zisizo za kiserikali na kusisitiza kuwa, lengo ni kuimarisha uwajibikaji katika sekta za umma.

“Lengo la Serikali ni kuimarisha uwajibikaji kwa umma na utendaji unaosisitiza ushirikiano kati ya Serikali na tasisi zisizo za kiserikali ili Watanzania wapate huduma bora nchini,” alisema.

Bw. Mkwizu ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. George Yambesi, alisema mkutano huo unafaida kubwa ambazo zitapatikana kama Serikali itashirikiana na asasi husika kuimarisha majadiliano kuhusu ubora na huduma zinazotolewa na Serikali kwa wananchi.

“Umefika wakati wa kutathmini utendaji kazi wa watumishi wa umma kupitia maoni ya wananchi, utaratibu huu utaisaidia Serikali kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utoaji maamuzi hasa kwenye sera zinazohusu huduma kwa jamii ili kukosoa na kuboresha,” alisema Bw. Mkwizu.

Alisema ushirikiano mzuri uliopo kati ya asasi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuboresha utoaji huduma kwa wananchi ambao kama watafahamu haki zao, itawarahisishia kuzidai kwa watumishi ambao hawatekelezi majukumu yao.

“Ni ukweli usiopingika kuwa kushirikisha watendaji na wadau muhimu ambao wanahudumia wananchi, kutasaidia kurahisisha na kuharakisha mabadiliko ya kiutendaji serikalini,” alisema.

Bw. Mkwizu alikiri kuwepo changamoto katika utoaji taarifa sahihi kwa wananchi hivyo Serikali imeunda Bodi ya Mshahara ili iweze kusimamia na kuboresha mishahara katika sekta za umma.

Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu katika sekta ya afya-SIKIKA Bi. Lydia Kamwaga, alisema upatikanaji wa taarifa kwa wakati ni mgumu kutokana na ukosefu wa matamko ya kisera, miongozo ya Serikali kwa watumishi wa Serikali.

Alitoa wito kwa Serikali kuwepo na mafunzo juu ya wajibu kwa watumishi wa Serikali katika kuhudumia wananchi na kukusanya taarifa kwenye taasisi za Serikali ziboreshwe.  

Bi. Kamwaga alisema hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya taasisi na watumishi wa Serikali wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma.


No comments:

Post a Comment