26 July 2012
CHADEMA yavuna 256 Kilomero
Na Rehema Maigala
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, kimevuna wanachama wapya 256, waliohamia chama hicho kutoka vyama vingine vya siasa.
Wanachama hao wametoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF), na Tanzania Labour Party (TLP), ambao walirudisha kadi zao kwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), Bw. John Heche, alipokuwa jimboni humo kwenye ziara ya muendelezo wa vuguvugu la mabadiliko M4C.
Bw. Heche aliwapokea wanachama hao katika mikutano minne aliyofanya Kata za Ifakara, Mang’ula, Msolwa na Mkamba ambao kati ya hao, 214 wanatoka CCM, 28 CUF na 14 TLP.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao, aliyekuwa Balozi wa nyumba 10, Kata ya Mkamba, Bw. Mussa Katanduki, alisema ameamua kuondoka CCM baada ya chama hicho kukosa mwelekeo na maadili ya uongozi.
Alidai CCM kwa sasa kinakumbatia ufisadi ambapo katika kipindi chote cha utawala wao, wameshindwa kuwaondoa maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini hivyo kusababisha maisha ya Watanzania hasa waishio vijijini kuwa magumu.
“Sisi wakazi wa vijijini ndio tunaoteseka, hatuna kitu ambacho tunategemea zaidi ya kilimo sasa pembejeo zenyewe bei juu hivyo kusababisha kilimo chetu kuwa cha kizamani,” alisema.
Mratibu wa ziara hiyo, Bw. Azizi Himbuka, alisema huo ni mwanzo katika kuhakikisha CHADEMA kinajipanga vyema kwenye uchaguzi wa vijijini na vitongoji.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika hivi karibuni baada ya kutangazwa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
“Sisi CHADEMA bado tupo imara kwa ajili ya kutetea haki za Watanzania hasa waishio vijijini, tutahakikisha kile tunachoahidi kwa wananchi lazima kitekelezwe,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment