18 July 2012

Jeshi la polisi liungwe mkono kutokomeza uhalifu



Na Goodluck Hongo

USALAMA ni jambo muhimu katika maendeleo ya mtu na Taifa kutokana na umuhimu wake.

Nchi yenye usalama inakuwa na amani na hivyo kuwa kimbilio la wawekezaji na wazawa kufanya biashara na shughuli nyingine za maendeleo bila woga.


Hali hiyo imelifanya jeshi la polisi limekuwa likipambana kufa na kupona na kukabiliana uso kwa uso na majambazi yanayotumia silaha za moto ili kuwalinda wananchi na mali zao.

Pamoja na juhudi hizo, ushirikiano wa raia ambao ni wananchi katika kutoa taarifa na kuwafichua wahalifu unahitajika ili kuhakikisha kuwa usalama unakuwepo na kutokomeza matukio ya uhalifu.

Mfano halisi ni katika jiji la Dar es Salaam hakuna sehemu iliyokuwa hatari  kwa uhalifu  kama  Temeke  ambapo kulikuwa kundi kubwa la uhalifu lililojulikana kama mbwa mwitu na kuzua hofu kwa wananchi.

Wakazi wa keko walikosa amani kutokana na kasi ya uhalifu kuongezeka hasa uvunjaji wa nyumba huku wakihofia usalama wao baada ya kuporwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke ACP David Misime anasema kuwa hali ya Keko inaridhisha kwani kutoka matukio 30 ya uvunjaji kwa siku yamepungua hadi kufikia matukio mawili, kwa siku kwa hili lazima tulipongeze jeshi hilo katika juhudi zake za kupambana na uhalifu.

Wananchi lazima waunge mkono juhudi hizo katika wilaya yao kutokomeza uhalifu na kuiunga mkono sera ya ulinzi shirikishi ambayo Kamanda Misime anaifanya kila sehemu hadi katika shule za msingi ikiwa ni hatua ya kutokomeza uhalifu.

Ingawa juhudi hizo zinafanywa ili kuwahamasiha wananchi kuwafichua wahalifu lakini wananchi waelewe kuwa jukumu la ulinzi si la jeshi la polisi peke yake kwani bila wao matukio  hayo hayawezi kuisha.

Wananchi wa Temeke mmeona jinsi jeshi hilo linavyofanya kazi lakini lazima muelewe na kukubali kuwa peke yao hawawezi kwa kuwa polisi ni wachache na eneo linalohitajika kupata ulinzi ni kubwa hivyo bila aibu wala woga lazima muwafichue wahalifu kwani kwa kufanya hivyo mtaweza kuishi salama bila hofu kama mnavyoishi sasa hivi.

Athari za kuibiwa ni kubwa kwani zinarudisha nyuma maendeleo kama mtawaogopa kuwafichua basi mjue kabisa si kila kosa ni uzembe wa polisi kuchelewa eneo la tukio lakini pia na nyie raia msipowafichua mapema wakati kila siku mnawaona  na kupishana nao mtaani.

Katika vita hii wananchi mnatakiwa kuweka pembeni undugu na ujirani kwani usalama ni muhimu kwa jamii nzima.

Kwa sasa vibaka wameongezeka wakipora vitu vidogo vidogo zikiwemo nyaya za umeme. Naamini kuwa watu hawa wanajulikana katika jamii hivyo ni wakati muafaka kuwafichua.

Nionavyo, hali ya usalama jijini sio mbaya sana ukilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita ambapo uhalifu wa kutumia silaha unafanywa hadharani hadi kufika hatua wananchi kulalamika kuwa hata baadhi ya askari wa jeshi la polisi wanahusika katika kufanya uhalifu kwani mamilioni ya pesa yaliibiwa kwa mtutu wa bunduki.

Hakuna ubishi kuwa kwa sasa askari atakayekwenda kunyume na sheria na kanuni za jeshi hilo atafukuzwa kazi kama wengine walivyofukuzwa na kufikishwa mahakamani hizo ni hatua zinazochukuliwa na jeshi la polisi kukabiliana na hali ya uhalifu hivyo lazima liungwe mkono kwa nguvu zote.

Binafsi nalipongeza jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke chini ya Uongozi wake ACP David Misime kwa kuweza kusafisha vichaka na makazi ya majambazi yaliyokuwa tishio kwa wananchi likiwemo kundi hatari la mbwa mwitu.

Pia Wilaya hiyo ni kubwa hivyo juhudi zako za kuhimiza ulinzi shirikishi ziendelee lakini pia lazima liwashughulikie askari ambao wamekuwa wakilalamikiwa  na wananchi na kuwachukulia hatua.

Pamoja na hali hiyo jeshi la polisi lisibweteke na liongeze nguvu na kutoa motisha kwa askari wanaofanya vizuri katika utendaji wao wa kazi ili kuongeza mori na ari katika kutekeleza majikumu yao.

Watanzania tuelewe kuwa kama kazi imefanyika vyombo vya habari ni wajibu wetu kueleza mazuri lakini sio kuyapa nafasi mabaya tu kwani wapo wengi waliofanya mazuri katika nchi hii lakini watanzania wengi hawawajui zaidi ya kuwajua kwa upana mafisadi.

Nilazima suala la ulinzi shirikishi liungwe mkono na wananchi wote kwani waathirika wakubwa ni wananchi wenyewe hivyo ni jukumu letu kushirikiana na jeshi la polisi katika kutokomeza uhalifu.

No comments:

Post a Comment