26 July 2012

Flying Eagles wawasili kuivaa Ngorongoro J.pili



Na Janath Abdulahim

TIMU ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Nigeria (Flying Eagles) imewasili nchini jana kwa ajili ya mechi yao ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za 18 za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazochezwa mwakani nchini Algeria.

Timu hiyo iliwasili jana kwa ndege ya Rwanda ikiwa na msafara wa watu 30 wakiwemo wachezaji 18.

Flying Eagles itapambana na Ngorongoro Heroes katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mechi hiyo itachezeshwa  na waamuzi kutoka Kenya wakati Kamishna ni Charles Masembe kutoka Uganda.

Flying Eagles inayofundishwa na kocha John Obuh, jana juzi ilicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali. Nigeria ililala kwa bao 1-0.

Msafara wa timu hiyo unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF), Chris Green.

Baadhi ya wachezaji walioko katika kikosi cha Flying Eagles ni Chidi Osuchukwu, Alhaji Gero, Shehu Abdullahi, Aminu Umar, Aliyu Mohamed, Uche Agbo, Jonah Usman, Harrison Egbune, Hassan Abubakar na Yahya Adamu.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A itakuwa sh. 10,000.

No comments:

Post a Comment