27 June 2012

Yondani 'out' siku mbili Yanga *The Express kupima vifaa vipya


Na Zahoro Mlanzi

BEKI mpya wa mabingwa wa Kombe la Kagame Yanga, Kelvin Yondani atakosa mazoezi ya siku mbili kutokana na kuwa na udhuru huku viungo Nurdin Bakari na Nizar Khalfan wameumia  mazoezini.

Mbali na hilo, timu ya The Express kutoka Uganda inatarajiwa kutua nchini Jumamosi kwa ajili ya kuwapima wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya mashindano mbalimbali.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Louis Sendeu alisema Yondani atakosa mazoezi kwa siku hizo baada ya kupewa ruhusu kutokana kuwa na mambo binafsi anayashughulikia.

"Ni kweli Yondani leo (jana) hakuwepo mazoezi, lakini ni mzima ila ana udhuru ambao aliufuata uongozi na kuuleza na ikaamuliwa aruhusiwe na tunatarajia Alhamisi (kesho) ataendelea na mazoezi kama kawaida," alisema Sendeu.

Pia alizungumzia kukosekana mazoezini kwa nahodha, Shadrack Nsajigwa ambaye naye ana matatizo ya kifamilia huku Nizar na Nurdin walifanya mazoezi lakini wakaumia.

Alisema wachezaji hao wamepewa mazoezi maalumu kutokana na majeraha waliyoyapa, hivyo hawatakuwepo katika programu ya kocha Fredy Felix 'Minziro', mpaka watakapopona.

Akizungumzia ujio wa kiungo Haruna Niyonzima, Sendeu alisema walitarajia jana angewasili na leo asubuhi kuanza mazoezi na wenzake.

Katika hatua nyingine, Minziro akizungumzia kuhusu mechi za kujipima nguvu, alisema wamefanya mazungumzo na The Express ya Uganda na wameahidiwa watakuja nchini na watacheza nayo Jumamosi.

Alisema mechi hiyo ni moja ya mechi ambazo wamepanga kucheza za kirafiki za kimataifa kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la Kagame litakalofanyika Julai 14, mwaka huu.

Wakati huohuo, mshambuliaji mpya, Said Banahuzi ameibuka nyota wa mazoezi baada ya kuonesha kiwango cha juu katika upachikaji mabao na kufanya mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo kumshangilia mazoezi yalipoisha.

No comments:

Post a Comment