26 June 2012
Mbunge atoa mpya bungeni *Pinda apiga marufuku magari ya kifahari *Lengo ni kupunguza matumizi serikalini
Na Benedict Kaguo, Dodoma
MBUNGE wa Ludewa, Bw. Deo Filikunjombe (CCM), ameshauri fedha za rada zilizorejeshwa nchini na Serikali ya Uingereza, zitambulike kama “Rushwa ya Rada”, badala ya chenji ya rada.
Bw. Filikunjombe aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma baaada ya kuomba mwongozo wa Spika wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia, akiwasilisha mapitio ya kazi kwa mwaka wa fedha 2011/12 na mwelekeo wa kazi kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Alisema ili kuweka kumbukumbu kwa Taifa ni vyema fedha hizo zikaitwa “Rushwa ya Rada” na Serikali ifafanue kwanini zikarudishwa kwa ajili ya kumbumbuku za vizazi vijavyo.
Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, alikataa mwongozo huo na kumtaka Bw. Filikunjombe kuuliza swali hilo atakapopata nafasi ya kuchangia katika Wizara hiyo.
Hata hivyo, Bi. Ghasia alisema Serikali ilipokea fedha za fidia ya ununuzi wa rada kiasi cha paundi milioni 29.5, kutoka Serikali ya Uingereza sawa sh. bilioni 72.3 za Kitanzania ambazo zitatumika kuimarisha sekta ya elimu ya msingi nchini.
Alisema kati ya fedha hizo sh. bilioni 54.2 zitatumika kununua vitabu vya kiada kwa shule na sh. bilioni 18.1, kutengeneza madawati kwa shule za msingi.
“Madawati ambayo yatapatikana, hakitoshi lakini kitasaidia kupunguza tatizo kubwa la madawati nchini, ujenzi wa baa na nyumba za kulala wageni karibu na maeneo ya shule kuanzia sasa ni marufuku, naziomba halmashauri zote nchini kusitisha vibali vyote vilivyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo haya,” alisema.
Alisema ipo changamoto ya maeneo ya shule kuvamiwa na wafanyabiashara hasa katika maeneo ya mijini na kutumia mikataba isiyo halali kujenga vibanda vya biashara kuzunguka shule husika.
Kutokana na hali hiyo, Bi. Ghasia amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali Januari 15,2010 kuhusu udhibiti wa biashara maeneo ya shule.
Wakati huo huio, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, amepiga marufuku ununuzi wa magari ya kifahari serikalini ili kupunguza matumizi yasiyo na tija ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiigharimu Serikali
Bw. Pinda aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha mwelekeo wa kazi za Serikali, makadirio ya matumizi ya fedha katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Alisema kuanzia sasa, hatua zaidi zitachukuliwa kwa kuweka ukomo wa ukubwa wa injini za magari ambayo yanaweza kununuliwa na Serikali Kuu, taaasisi zake na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aliongeza kuwa, chini ya utaratibu huo, magari yatakayonunuliwa hayatazidi ukubwa wa injini wa CC 3,000 ambapo kwa viongozi na watendaji wakuu, ambapo kwa watumishi wengine ambao wanastahili kutumia magari ya Serikali yatakuwa CC 2,000.
“Ili kupunguza matumizi ya magari kwa viongozi na watendaji wakuu kwa safari za mikoani, Serikali itaanzisha vituo vya Kanda vya magari ya Serikali au kila ofisi itatenga magari machache ambayo yatatumika mikoani kwa shughuli za kikazi,” alisema.
Alisema mpango huo ukikamilika, Serikali itapunguza matumizi ya fedha kwa kiwango kikubwa ili kupunguzi matumizi yasiyo na tija ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wabunge.
Aliongeza kuwa, katika mkutano wa saba wa Bunge uliofanyika Aprili mwaka huu, alitoa ahadi ya Serikali kufanyia kazi maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na wabunge walipokuwa wakijadili taarifa mbalimbali za Kamati za Kudumu za Bunge.
Taarifa hizo ni zile za Kamati inayohusika na Hesabu za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo ziliainisha hoja mbalimbali za ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka 2009/10.
Alisema katika bunge hilo, alieleza jinsi Serikali itakavyochukua hatua kwa watendaji wote waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wa mali ya umma kama watathibitika kutenda makosa.
Bw. Pinda alisema, Serikali imeziagiza mamlaka zake mitaa kupitia taarifa na hoja zote za ukaguzi za mwaka 2009/10, zilizotolewa na CAG na kuzitafutia majibu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili mwaka huu.
“Baada ya mchakato huu kukamilika, taarifa hizi zitawasilishwa ngazi ya Mkoa kupitia majibu ya hoja husika na kuziwasilisha kwa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
“Taarifa za mikoa na halmashauri zote, zitawasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kabla ya Novemba 2012 ili kuandaa majibu ya pamoja na kuyawasilisha bungeni,” alisema Bw. Pinda.
Alisema watumishi wa umma ambao watatuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha, watachunguzwa na wakibainika watavuliwa madaraka waliyonayo na kufikishwa mahakamani ambapo Serikali haitawahamisha watumishi wa aina hiyo, bali hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi.
“Nawaagiza Wakurugenzi watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kubandika kwenye mbao za matangazo Makao Makuu ya Halmashauri na kwenye vituo vyote vya utoaji huduma, fedha zinazopokelewa kila mwezi na matumizi yake.
“Hii itawezesha wananchi kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya huduma katika maeneo yao, katika mwaka wa fedha 2012/13, Ofisi yangu na taaasii zake tunatarajia kutumia zaidi ya sh. bilioni 176.7,” alisema.
Maboresho ya Sekta ya Fedha
Alisema Taasisi za Fedha zina mchango mkubwa wa kuchochea maendeleo na ukuaji uchumi ambapo kwa kutambua mchango huo, Serikali inatekeleza Programu ya Maboresho ya Sekta ya Fedha, ambayo imekuwa na mafanikio ya kuridhisha.
Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la idadi ya taasisi hizo ambazo hadi sasa zimefikia 49, zikiwa na matawi 519 chini kote. Taasisi hizo pia zimeonesha mafanikio makubwa katika eneo la huduma za kibenki kwa njia ya mtandao.
Sensa ya Watu na Makazi 2012
Bw. Pinda alisema, maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo itafanyika Agosti 26 mwaka huu, yamekamilika ili kutekeleza mpango wa maendeleo ya nchi.
Alisema katika awamu ya kwanza, kazi zilizofanyika ni kutenga maeneo ya kuhesabia watu, kutayarisha madodoso na miongozo mbalimbali, kufanya Sensa ya majaribio, kununua vitendea kazi, kuchapisha nyaraka na kuunda Kamati za Sensa za Mikoa, Wilaya.
“Kazi inayoendelea sasa ni uhamasishaji wa kutoa elimu kwa umma ili kila mwananchi ashiriki kikamilifu, shughuli nyingine ni utoaji mafunzo kwa makarani, wasimamizi, usambazaji vifaa na kuingiza takwimu katika kompyuta,” alisema.
Kuimarisha Demokrasia na Muungano
Alisema kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi kushiriki masuala ya kisiasa. Hali hiyo inaashiria kukua kwa Demokrasia nchini, vyama vipya vya siasa vimeendelea kusajiliwa na vilivyopo kujiimarisha zaidi.
Aliongeza kuwa, mwaka 2011/2012, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imepokea maombi ya kusajili vyama vipya viwili, Chama cha Kijamii (CCK), ambacho kimepata usajili wa kudumu na kufanya idadi ya vyama vyenye usajili wa kudumu kufikia 19.
Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimepata usajili wa muda na Chama cha Movement for Democratic and Economic Change, kinaendelea kufanyiwa uhakiki.
Bw. Pinda alisema, Ofisi ya Msajili itaendelea kushughulikia maombi ya usajili wa vyama, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfumo wa vyama vingi vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010.
Pia itafuatilia uhai wa vyama husika kwa mujibu wa Sheria na kuanzisha Ofisi mbili za Kanda ambazo ni Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na Kanda ya Magharibi mikoa ya Tabora, Kigoma, Shinyanga na Katavi.
Mabadiliko ya Katiba
Aliongeza kuwa, Novemba 2011, Bunge lilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 8 ya Mwaka 2011 (Sura ya 83) na kufanya marekebisho ya Sheria hiyo katika Mkutano wa Bunge la Sita, Februari 2012.
Hatua hiyo, ilimwezesha Rais Jakaya Kikwete baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein, kuteua Wajumbe wa Tume itakayoratibu na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba.
Alisema tume hiyo ina wajumbe 32 ikijumuisha wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii kutoka pande mbili za Muungano.
“Tume imeanza kazi rasmi Mei mosi mwaka huu, Serikali imefanya maandalizi muhimu ya kuiwezesha tume kufanya kazi yake ipasavyo pamoja na kuipatia vifaa vya kisasa vya kukusanya, kutunza kumbukumbu na kufungua tovuti,” alisema.
Aliongeza kuwa, Mpigachapa Mkuu wa Serikali imepewa jukumu la kuchapisha kwa wingi Katiba na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili wananchi waweze kuelewa na kutoa michango yao kwa uhakika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Namuunga mkono Mhe. Flikunjombe kuwa fedha za rada ziitwe "Rushwa ya Fedha za Rada" na waliohusika na kashfa hii wachukuliwe hatua.
ReplyDeleteNIWASHUKURU WABUNGE WOTE KUJALI CAUCAS ZAKE HUU NDIO MSINGI WA DEMOKRASIA YA VYAMA VINGI IWAPO UTAOMBA RIDHAA KUPITIA CHAMA CHAKO KURUDI BUNGENI NI VEMA KUZINGATIA CAUCAS ZA CHAMA CHAKO KILICHOKUPA RIDHAA YA KUGOMBEA NA KUKUKAMPENIA UKASHINDA KWA KUWA HAKUNA MGOMBEA BINAFSI SIDHANI KILA MTU ANA ILANI YAKE KUPINGANA NA CAUCAS YA CHAMA CHAKO SIJUI KUNA FAIDA AU HASARA
ReplyDeleteRushwa itaimaliza Tanzania hii ni rushwa moja tu mabilioni ya fedha yamepatikana na nuanga mkono hiyo kuitwa rushwa ya rada na rushwa nyengine zichunguzwe na pesa zirydishwe
ReplyDelete