27 June 2012

Waliofilisi Mashirika wanyongwe-Mbunge *Adai kama wamekufa makaburi yafungwe pingu *Ni TRL, ATCL na NIC, TAKUKURU lawamani


Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, mkoani Rukwa, Bw. Ally Kessy (CCM), ameitaka Serikali iwachukulie hatua watumishi waliohusika kufilisi mashirika ya umma pamoja na kuwanyonga.

Alisema kama itabainika wahusika wameshatangulia mbele ya haki (kufa), makaburi yao yafungwe pingu kama ishara ya kukasirishwa na hujuma kubwa walizoifanyia nchi.

Bw. Kessy aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kusisitiza kuwa, watumishi hao ni pamoja na waliofilisi Shirika la Reli nchini
(TRL), Shirika la Ndege (ATCL) na Shirika la Bima la Taifa
(NIC) kwa kuliingizia Taifa hasara kubwa.

Alisema tatizo la ufisadi unaoendelea unachangiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kishindwa kuwajibika ipasavyo.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka Serikali kuwachunguza watumishi wa TAKUKURU, akidai kuwa, wanapopelekewa kesi wanawapigia simu watuhumiwa na kuwaeleza fulani ndiye ametoa taarifa hizo.

Bw. Kessy alisema mara kadhaa taasisi hiyo imekuwa ikiwaomba wananchi waisaidie kuwapa taarifa za rushwa kana kwamba wao hawawaoni watumishi wala rushwa.

“Serikali hata ikiwa na mipango mizuri kiasi gani, kama itashindwa kuwadhibiti wala rushwa, shughuli za maendeleo hazitaweza kutekelezwa, suluhisho si kumsimamisha mtu kazi au kuhamishwa, anapaswa kukamatwa na kunyongwa.

“Wananchi wa Nkasi Kaskazini wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ya afya, elimu na ukosefu wa miundombinu mizuri ya usafiri, sheria zilizopo sasa zinaonekana kuwalinda wezi hivyo hatua zichukuliwe ili kuwezesha fedha zinazopotea zitumike kwa maendeleo kuliko ilivyo sasa,” alisema Bw. Kessy.

Aliongeza kuwa, bila kufanya hivyo ni sawa na kuwadanganya wananchi na kuwapa matumaini ambayo hayapo.


1 comment:

  1. SHERIA YA KUNYONGA WATU IKO CHINA WANANYONGA KWA SABABU WAKO WENGI WENGI KINACHOTUSUMBUA NI USHAMBA KATIKA KUINGIA KWENYE UTANDAWAZI TUKUMBUKE UJAMAA HAUPO TENA NA SITEGEMEI TUTARUDI HUKO

    ReplyDelete