28 June 2012

Simba kuwatoa kwa mkopo Machaku, Shamte *Jabu, Kago, mikataba yao imekwisha


Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeanika majina ya wachezaji walioachwa na waliositishiwa mikataba yao kwa timu mbalimbali huku Klabu ya Simba, itawatoa kwa mkopo Rajab Isihaka, Salum Machaku, Haruna Shamte na Shija Mkina.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura ilieleza kwamba mbali na hao pia wachezaji Ally Mustafa, Derick Walulya, Gervais Kago na Juma Jabu wamemaliza mikataba yao wakati Salum Kanoni mkataba wake utamalizika Juni 30, mwaka huu.

Alisema timu hiyo imewasilisha majina ya wachezaji hao wanne ambao bado wana mkataba na timu hiyo wakiwa na lengo la kutaka wakaongeze viwango vyao.

"Mbali na Simba, pia Azam FC imekatisha mikataba ya wachezaji watatu ambapo ni Tumba Swedi, Mau Bofu na Sino Augustino," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Alisema Polisi Morogoro iliyopanda msimu huu imeacha wachezaji 17, wakati Tanzania Prisons ambayo pia imepata hadhi ya ligi msimu huu imeacha wachezaji 11.

Wambura alisema kwa upande wa Kagera Sugar, wachezaji 12 wamemaliza mikataba yao na kwamba uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 na utamalizika Julai 30, mwaka huu wakati kipindi cha kuacha wachezaji (kwa wasio wa Ligi Kuu) ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment