27 June 2012

Vigogo 'wezi' watajwa *Wadaiwa kuhujumu mikoa ya kusini



Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalumu, mkoani Lindi, Bi. Riziki Lulinda (CCM), amewataja kwa majina baadhi ya vigogo waliopo katika halmashauri nchini wanaodaiwa kufanya wizi wa mabilioni ya fedha na kuhamishiwa vituo vya kazi hali inayochangia kukwamisha maendeleo hasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Bi. Lulinda aliwataja vigogo hao bungeni mjini Dodoma jana wakati akichangia bajeti ya Waziri Mkuu akiwa na nyaraka mkononi.

Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watumishi waliochangia kurudisha nyuma maendeleo, bado wameendelea kupewa madraka kwa kuhamishwa vituo vya kazi na kusisitiza kuwa, watumishi hao wametoka mikoa ya Kaskazini.

“Hawa watumishi wanafanya mikakati maalumu ya kuihujumu mikoa ya Kusini ikiwemo Lindi na Mtwara ili ionekane wananchi wake wamechoka na hawawezi kupata maendeleo katika Nyanja mbalimbali zikiwemo barabara, huduma za afya na elimu.

“Bw. Joaquim Materu ambaye alikuwa Halmashauri ya Kilosa, aliiba sh. bilioni 1.1 na kupewa adhabu ya kuhamishiwa Mkoa wa Lindi ili aendelee kuwahujumu wananchi wa Mkoa huu.


“Pia yupo Eunice Maro ambaye alikuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Kilosa ambaye aliiba sh. milioni 262 ambazo aliziingiza katika Benki ya NMB, namba 206660017 inayosomeka kwa jina la  Lugemalila lakini Serikali imempa uhamisho kwenda Mkinga,” alisema Bi. Lulinda.

Aliongeza kuwa, mwingine ni R.R Ndaskoi ambaye aliiba sh. milioni 23, na baadae aliiba tena sh. milioni 30, akishirikiana na Bw Materu na kuhamishiwa Halmashauri ya Ngorongoro .

Bi. Lulinda alisema, mtumishi mwingine ni Mlaki ambaye aliiba sh. bilioni 6 wakati akiwa Halmashauri ya Kishapu na kuhamishiwa Babati akihusisha hujuma hizo na kabila la wachaga.

Hali hiyo ilisababisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Bw. William Lukuvi, kuomba mwongozo wa Spika akidai Bi. Lulinda alitumia lugha za ubaguzi, udini na ukabila ambazo haziruhusiwi ndani ya Bunge.

Mwenyekiti wa Bunge Bi. Jenister Mhagama, alimtaka Bi. Lulinda kufuta kauli ya Wachaga kuihujumu mikoa ya Kusini na kukubali kufanya hivyo lakini alisisitiza kuwa, Serikali iache mchezo wa kushughulikia wabadhirifu kwani nchi inakosa maendeleo hasa mikoa ya Kusini kutokana na watu wa aina hiyo.

1 comment:

  1. MTOA HOJA NI MKABILA ALIOWATAJA NI WA KABILA MOJA TU WACHAGGA WAMEPATA AJIRA NI KWA SABABU NI RASILIMAWATU HAYATI MWL ALIKEMEA SANA UKABILA KWAMBA KARNE HII WATU WANAPANDA BASI LA UKABILA

    ReplyDelete