25 June 2012
Walemavu 90 wa macho wapewa mafunzo ya utambuzi wa katiba
Na Mwandishi Wetu
VIJANA 90 wenye ulemavu wa macho katika Wilaya za Temeke na Ilala, jijini Dar es Salaam, wamepatiwa mafunzo yanayohusu utambuzi wa katiba ya sasa ili kubaini kasoro zilizopo na kutumia fursa hiyo kutoa maoni yao katika mchakato wa Katiba Mpya.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Vijana wa Chama cha Wasioona nchini (TLB), Bw. Moshi Enos, alisema mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kikamilifu kutoa maoni yao.
“Changamoto inayowakabili watu wenye ulemavu wa macho ni kwamba, katiba zilizopo zimeandikwa kwenye maandishi ya kawaidia ambayo hawawezi kuisoma.
“Kimsingi walemavu wa macho hawaifahamu Katiba hii ndiyo maana tumeona tutoe mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze kuchangia kwa kutoa maoni yao kwenye Katiba Mpya,” alisema Bw. Enos na kuongeza kuwa, mafunzo hayo yamedhaminiwa na Mfuko wa Jamii wa The Foundation for Civil Society.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLB, Bw. Greyson Mlanga, alisema Serikali inapaswa kutafsiri katiba ya sasa katika maandishi ya nundu ili jamii hiyo iweze kuisoma.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa, watu wenye ulemavu wa macho nchini wapo 900,000 ambao wengi wao wamekosa fursa ya kusoma katiba iliyopo
“Wanaopata mafunzo haya ni wasioona 90 tu, wengi wao hawatabahatika kupata mafunzo haya na hawaijui katiba ya sasa, hivyo itakuwa vigumu kuchangia kwenye maoni ya Katiba Mpya,” alisema Bw. Mlanga.
Aliongeza kuwa, walemavu wa macho wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo wangependa ziingizwe katika Katiba Mpya pamoja na fursa ya kupata ajira.
Bw. Mlanga alisema waajiri wengi wanawanyanyapaa watu wenye ulemavu kwa kutowapa ajira hata kama wana sifa katika nafasi wanazoomba hivyo wanaamini Katiba Mpya, itaondoa tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi wa kudumu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment