21 June 2012
Katiba mpya iwe na dira ya maendeleo
Na Halfan Diyu
KATIBA muongozo ambao taifa lolote limejiwekea jinsi ya kuendesha shughuli za kila siku za taifa lao.
Taifa linakuwa imara linapokuwa na katiba imara na viongozi bora, wenye maono ya kuwaletea maendeleo wananchi wao.
Taifa lazima lisimamie misingi ya haki na ianishwe katika katiba kwani ni haki pekee huleta watu pamoja na kiondoa misingi yote ya unyonyaji.
Pia, ndio sheria mama nchini na katiba zote zinazotengenezwa na taasisi au vyama vya siasa zinapaswa kuakisi yale yote
yaliyopo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si kupingana, kinyume na hapo itakuwa batili.
Maendeleo ya nchi nyingi zilizoendelea yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa na katiba imara na inayokidhi mahitaji ya sekta mbalimbali kama za elimu, afya, utamaduni, uchumi, siasa, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa wananchi kuzungumza au kutoa maoni yake.
Hakuna ubishi kuwa nchi ya Marekani ni moja ya mataifa ambayo yamekuwa na katiba imara inayogusa sekta zote nilizotaja hapo juu na ambayo imedumu kwa muda mrefu bila
kufanyiwa marekebisho ya mara kwa mara.
Matokeo yake tunashuhudia Taifa hilo likisimama kwa muda mrefu kwa kuwa na uchumi imara duniani.
Nchini baada ya kuundwa kwa katiba mwaka 1977, tayari yameshafanyika marekebisho kumi na nne hadi mwaka 2005, ambapo ya kwanza yalifanyika mwaka 1979.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba nchini, Bw.Deus Kibamba anasema marekebisho ya kwanza ya mwaka 1979 yaliingiza moja ya mambo muhimu katika taifa letu, ambapo ni
kuanzishwa kwa Mahakama ya Rufaa.
Mwaka 1980 yalifanyika tena marekebisho katika Katiba na moja ya marekebisho hayo ni kuingizwa kwa katiba ya Zanzibar katika Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Mwaka 1982 yalifanyika marekebisho ya mfumo mpya wa kuchagua wakuu wa mikoa, mwaka 1984 marekebisho bora ambayo yalizingatia maoni ya wananchi ambapo suala la haki za binadamu liliingizwa katika katiba.
Hayo ni baadhi ya marekebisho machache tu ambayo yalifanyika katika hiyo miaka niliyoitaja hapo juu na kufikia hadi mwaka 2005 jumla ya mabadiliko kumi na nne yalifanyika na mengi yaligusa masuala ya siasa na muungano, achilia machache kama ya haki za binadamu ambayo yanagusa jamii yote bila kubagua.
Vilevile ubora na uimara wa katiba mpya ijayo uende sambamba na kudumu kwa miongo mingi na si kufanya marekebisho ya mara kwa mara ambayo yanagharimu fedha nyingi za walipa kodi.
Katika kipindi hiki Taifa lipo katika vuguvugu la kuanza mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya, ambapo ifikapo tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 2014 Katiba hiyo inatakiwa
iwe imekamilika.
Wananchi waelimishwe umuhimu wa kuchangia maoni ya masuala mbalimbali yanayogusa maisha yao ya kila siku na si kuwa na mawazo mgando ya kuchangia katika masuala ya
muungano na siasa tu, ingawa pia yana umuhimu katika mustakabali wa Taifa.
Nionavyo jamii inatakiwa kupata uelewa na nafasi ya kuchangia maoni yao ili kupatikana kwa katiba bora, imara itakayogusa sekta zote kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
KINACHOKATISHA TAMAA NI WIMBI KUBWA LA WATANZANIA WASIOJUA KUSOMA NA KUANDIKA IWAPO NI ZAIDI YA ASILIMIA 30% HAWAJUI KUSOMA KUANDIKA NA KUHESABU HIVI SIO MATUMIZI MABAYA YA RASILIMALIFEDHA KUCHAPISHA KATIBA AMBAZO HAZITASOMWA .WATU WA AINA HII WATACHANGIA NINI KATIKA MAREKEBISHO YA KATIBA NINA MASHAKA IWAPO HATA HILO WAZO LA KUTAKA KATIBA MPYA LIMETOKEA KWAO WENGI WANAIMBA WIMBO WASIOJUA MAANA YAKE TATIZO UPEO FINYU
ReplyDelete