27 June 2012
TAKUKURU waingia Maliasili, Nishati
Na Stella Aron
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), inatarajia kuwaburuta mahakamani maofisa wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa katika Wizara ya Maliasili na utalii, Nishati na Madini pamoja na Idara ya Pembejeo kwa kuisababishia Serikali hasara.
Ili kutimiza azma hiyo, tayari kesi 173 ziko katika hatua za mwisho kufikishwa mahakamani.
Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hoseah, aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika mahojiano Maalumu ya Kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV.
Alisema kufikishwa mahakamani kwa vigogo hao kunatokana na ripoti iliyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Aliongeza kuwa, kutokana na ripoti ya CAG, taasisi yake imefanikiwa kufungua kesi 73 zinazotokana na ulipaji wa mishahara hewa ambazo kati ya hizo, 32 zinawahusu Maofisa wa Wizara ya Maliasi na Utalii.
Dkt. Hoseah alisema, kesi zingine 63 zinahusu ulipaji wa pembejeo na kesi tano zinahusu Wizara ya Nishati na Madini.
“Tumeweza kupata mafanikio mengi katika kipindi cha miezi sita, tumeweza kufungua kesi tano zinazohusu manyangumi (vigogo), uchunguzi bado unaendelea kuhakikisha kuhakikisha manyangumi wote wanaojihusisha na rushwa wanafikishwa mahakamani,” alisema.
Alisema TAKUKURU imebaini kuwepo ubadhirifu mkubwa katika ulipaji mishahara hewa kwani wapo baadhi ya walimu wanaidai Serikali sh. milioni 2.6, lakini baadhi ya watumishi wasio waaminifu wamewaandikia sh. milioni 20.6.
“Huu ni ubadhifu mkubwa, ripoti ya CAG imetuwezesha kubaini vitendo vya rushwa katika ngazi mbalimbali, tutaendelea na mapambano mbali ya changamoto zilizopo,” alisema.
Aliongeza kuwa, ili kuhakikisha rushwa inadhibitiwa nchini wanatarajia kufungua matawi kwenye ofisi za kata ambayo yatawawezesha wananchi kushirikiana na taasisi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment