28 June 2012

Tamasha la filamu kufanyika Tanga



Na Victor Mkumbo

TAMASHA la Filamu la Tanzania Film Festival linatarajia kufanyika Juni 30, mpaka Julai 6 mwaka huu Jijini Tanga.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Kinywaji cha Grand Malt ambao ndiyo wadhamini wa tamasha hilo, Consolata Adam alisema tamasha hilo linatarajia kuwa la aina yake kwa mwaka huu kutokana na maandalizi.

Alisema wakazi wa Tanga, wameonekana kupenda tamasha hilo kutokana kupata burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wa filamu nchini.

Adam alisema tamasha hilo kwa mwaka huu limeboreshwa, ambapo pia litashirikisha wasanii wote wanaotamba katika tasnia ya filamu nchini.

Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butallah alisema tamasha hilo linaandaliwa na Kampuni ya Sofia Records ambapo hufanyika kila mwaka.

Alisema lengo kubwa ni kuwakutanisha wasanii pamoja na wadau mbalimbali wa sanaa za filamu nchini.

Butallah alisema tamasha hilo linatarajia kuwa la aina yake, ambapo pia wanajipanga kulifanya kimataifa zaidi ili kuweza kutangaza kazi za wasanii wa Tanzania nje ya nchi.

"Tunatarajia kuwa tamasha la mwaka huu litakuwa la aina yake na kuanzia mwakani litahama katika mikoa mingine" alisema.

Naye Mkurugenzi wa Sofia Records, Mussa Kissoky alisema anawashukuru TBL kupitia kinywaji cha Grand Malt kwa kuendelea kulidhamini tamasha hilo.

Alisema wanatarajia mashabiki wao watapenda kazi wanazofanya kutokana na ubunifu mkubwa kwa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment