28 June 2012

Mapya yaibuka kesi ya kusafirisha watu


Na Rehema Mohamed

UPANDE wa mashtaka kwenye kesi ya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, umeieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa walalamikaji walisafirishwa kutoka Yemeni kuja Tanzania kwa msaada wa Shirika la Kimataifa Uhamiaji (IMO).


Kesi hiyo inamkabili mfanyabiashara wa Mjini Arusha, Bw.Salim Ally anayedaiwa kuwasafirisha Bw. Abduswamad Zakaria, Bw. Hamidu Biabato, Bw. Raufu Biabato na Bw. Sadick Almas.

Wakili wa Serikali Bw. Hamidu Mwanga, aliyasema hayo jana mbele ya Hakimu Bw. Ilvin Mugeta, wakati kesi hiyo ilipoitwa ili mshtakiwa huyo aweze kusomewa maelezo ya awali.

Alidai walalamikaji walisafilishwa na mshtakiwa hadi nchini Yemen ili wakamjengee nyumba yake ya ghorofa tatu kuoneshwa michoro ya jengo na kusaini mkataba wa ujenzi.

Iliongeza kuwa, hali ilikuwa tofauti baada ya kufika Yemeni ambapo mshtakiwa hakuwapa mkataba wa ujenzi badala yake aliwapokonya hati zao za kusafiria na kuwalazimisha kujenga jengo hilo kwa lazima ili aweze kuwapa malazi na chakula.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, walalamikaji walilazimika kujenga jengo hilo kuanzia Septemba 2010 hadi Julai 2011, bila ya malipo.

Ilidaiwa kuwa, baada ya kuona mateso hayo, mmoja kati ya walalamikaji alifanikiwa kuwasiliana na ndugu yake aliyepo nchini ambaye alitajwa kwa jina la Kanali Lubinga wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambaye aliwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa  ambao nao kuwasiliana na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini Juni 14,2011.

Juni 22,2011 Wizara ya Mambo ya Nje iliwasiliana na IMO ambapo Julai mwaka huo, shirika hilo lilifanikiwa kupata mahali ambapo walalamikaji walikuwa wakifanya kazi na kuwarudisha nchini kwa matakwa ya mshtakiwa.

Ilielezwa kuwa, walalamikaji walifanikiwa kurudi nchini Julai 23,2011 na hatimaye taarifa za tukio hilo kufikishwa polisi.

Mshitakiwa alipoulizwa kuhusu madai hayo, alikubali kuwahi kukutana na mlalamikaji Bw. Abdulswamad mjini Arusha, kumpa fedha, kuwahifadhi nchini Yemen na kupokea barua kutoka Wizara ya Mambo ya Nje kuhusu malalamiko ya walalamikaji.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 16 hadi 19 itakapoletwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.

No comments:

Post a Comment