28 June 2012

Mwanafunzi abakwa na mjomba wake


Na Abdallah Amiri, Igunga

JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Makomero, Kata ya Igunga Mjini, Bw. Nzogya Ramadhani (38), kwa kosa la kumbaka mtoto wa dada yake (jina linahifadhiwa), mwenye umri wa miaka 12, anayesoma darasa la tano katika Shule Msingi Makomero.


Akizungumza na Majira, Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Mgaya Sena, amesema tukio hilo limetokea Juni 25 mwaka huu, saa 10 usiku na kumtaja mtuhumiwa kwa jina la Bw. Nzogya Ramadhani.

Alisema siku ya tukio, Bw. Ramadhani alitoroka nyumbani kwake kwa siri na kumuacha mkewe akiwa amelala na kwenda katika chumba walichokuwa wamelala  watoto.

“Alipofika kwenye chumba cha watoto, alisukuma mlango kwa nguvu na kufanikiwa kuingia ndani, baada ya kuingia ndani alimshika mtoto (jina tunalo) na kumtoa nje.

“Baadae alimuingiza jikoni na kuanza kumbaka akiwa amemziba mdomo na baada ya kumaliza unyama huo, aliondoka na kurudi chumbani kwake,” alisema Bw. Sena.

Mtoto huyo baada ya kufanyiwa unyama huo, alikwenda kwa shangazi yake na kumwambia mjomba wake amembaka hivyo hajisikii vizuri ndipo shangazi iliamua kupiga mbiu.

Wananchi walikusanyika na kutaka kumchoma moto mtuhumiwa lakini Bw. Sena alipiga simu Kituo cha Polisi Igunga ambao baada ya muda, askari walifika eneo la tukio wakiongozwa na Bw. Ame Alawi na kumkuta Bw. Ramadhani akiwa chini ya ulinzi.

Polisi waliondoka na mshtakiwa hadi kituoni ambapo mtoto huyo alikimbizwa Hospitali ya Wilaya kwa matibabu.

Kutokana na tukio hilo, baba wa mtoto Bw. Emmanuel  Razaro (54), alisema baada ya kusikia kitendo alichofanyiwa mwanae, yeye na ndugu zake walikaa na Bw. Ramadhani na kumuuliza kwanini ameamua kufanya unyama huo.

“Bw. Ramadhani alikiri na kusema kuwa, pombe alizokuwa amekunywa ndio zilisaababisha afanye kitendo hicho hivyo aliomba asemehewe,” alisema Bw. Sena.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi, Anthon Lutha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tayari wanamshikilia mtuhumiwa na atapandishwa kizimbani baada ya upelelezi kukamilika.

Alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kufanya vitendo vya ubakaji kwani Serikali haiwezi kufumbia macho na kuwapongeza wakazi wa Igunga kwa ushirikiano wao.

No comments:

Post a Comment